Kwa upande wa jiji la Dar es Salaam ambalo ndilo
lenye idadi kubwa ya waandishi nchini, maandamano hayo yameanza katika
kituo cha runinga cha Chanel Ten na kumalizikia katika uwanja wa
jangwani.
Akiwahutubia waandishi wa habari
waliohudhuria maandamano hayo, Nevil Meena ambaye ni katibu mkuu wa
jukwaa la wahariri nchini Tanzania amesema lengo la kufanya maandamano
ni kutumia njia wanazotumia watanzania wengine kueleza kero lao.
Hapo jana chama cha Upinzani nchini Tanzania
Chadema, kilimtaka rais Jakaya Kikwete kuunda tume ya kimahakama
itakayochunguza kifo cha mwandishi huyo kwa madai kwamba hawana imani na
kamati iliyoundwa na waziri wa mambo ya ndani kwa maelezo kuwa haina
mamlaka ya kisheria.
Huku mazingira yaliyopelekea kifo cha mwandishi
wa habari Daudi Mwangosi yakiwa bado yamegubikwa na utata, chama cha
Demokrasia na maendeleo kimewataka waziri wa mambo ya ndani Emmanuel
Nchimbi na mkuu wa jeshi la polisi Said Mwema kuachia ngazi mara moja
kama njia ya kuwajibika.
Mwenyekiti wa chama cha Chadema Freeman Mbowe,
amesema kuwa Chadema haina imani na kamati iliyoundwa na waziri Nchimbi
kwa madai kwamba imekosa mamlaka ya kisheria.
Hivyo amemtaka rais Jakaya Kikwete aunde tume ya
kimahakama itakayochunguza kifo cha mwandishi huyo na kwamba, iwapo
hayo hayatatekelezwa, chama hicho kitafanya maandamano makubwa.
Katibu mkuu wa jukwaa la wahariri nchini Nevil Meena amesema kuwa tukio la kuuawa kwa mwandishi huyo wa
habari marehemu Daudi Mwangosi tarehe mbili mwezi huu katika kijiji cha
Nyololo huko mkoani Iringa, kumeibua hisia kali miongoni mwa waandishi
wa habari pamoja na wanaharakati huku wengi wao wakihoji usalama wa
waandishi wanapokuwa kazini hasa katika mazingira magumu.
EmoticonEmoticon