UTI kwa wanawake?
NIMEPOKEA maswali mengi kuhusu tatizo la ugonjwa wa UTI kwa wanawake.
Inaonyesha kuwa ni tatizo linalowasumbua watu wengi nchini. Lakini pia
inaonyesha kuwa wengi wanashindwa kutofautisha UTI, kutokwa na uchafu na
kuwashwa sehemu za siri.
Wanaokuja kwa ajili ya matibabu hupewa elimu, lakini inaonyesha ni tatizo ambalo anayejua hawezi kumjulisha rafiki au jirani yake chanzo cha ugonjwa huo kwa sababu tu unahusiana na sehemu za siri. Si kila mwanamke yuko huru kusema kuwa aliwahi kupata tatizo sehemu za siri. Karibu nusu ya wanawake wote walishapatwa UTI na wengi huwarudiarudia kiasi kwamba inakuwa kero. Nikianza na UTI, napenda tufahamu maana yake kwanza, UTI ni kifupi cha maneno ya kiingereza Urinary Tract Infection (UTI), wazazi wengi wanaujua sana kwa sababu ya watoto chini ya miaka mitano husumbuliwa na ugonjwa huu. Maana halisi ya UTI kwa Kiswahili ni maambukizi katika njia ya mkojo. Napenda wanawake wanosumbuliwa na UTI wajue kuwa njia ya mkojo sio njia ya uzazi. Wapo wanaofikiri kuwa uke una njia moja ya uzazi na mkojo. Hapana. Njia ya mkojo inaachana na njia ya uzazi mwanzoni tu mwa uke. Uambukizo katika njia ya mkojo unapatikana kwa njia mbalimbali, tukiacha magonjwa ya kujamiiana, uambukizo wa njia ya mkojo unasababishwa na bakteria waishio ukeni au kwenye utumbo wa binadamu. Bakteria waishio ukeni hawana madhara ukeni, lakini wakihama na kuingia kwenye njia ya mkojo husababisha matatizo. Hii inaweza kutokea wakati wa ngono kwani wakati huo msuguano husababisha wale bakteria kutoka na majimaji na kufika kwenye tundu la mkojo na kuingia ndani. Wataalamu wanasema kuwa mwanamke anayefanya ngono mara kwa mara anaweza kuwa na UTI zaidi ya yule asiyefanya. Bakteria pia wanaweza kuhama kutoka sehemu ya haja kubwa na kuingia kwenye tundu la mkojo. Hutokea wakati wa kujisafisha na hasa kama mabaki ya kinyesi hubakia sehemu ya haja kubwa. Njia nyingine iwapo mwanamke atakuwa na tabia ya kubana mkojo kwa mda mrefu, kibofu cha mkojo kina misuli inayosadia mwanamke asiende kukojoa anapobanwa na mkojo mpaka atakapokuwa tayari. Iwapo atahisi kukojoa na asiende baada ya muda mrefu, ataichosha misuli ya kibofu kiasi kwamba hata siku anayokuwa na mkojo akikojoa hautoki wote na ule mkojo kidogo unaobaki kwenye kibofu huweka bakteria na kusababisha maambukizo. Dalili za UTI ni kujisikia kwenda haja ndogo mara kwa mara na utakapoenda unatoka mkojo kidogo tu. Utasikia mkojo ukichoma wakati unatoka na mwisho utasikia maumivu makali. Ikiendelea unaweza kusikia maumivu ya chini ya tumbo na kiuno. Hata hivyo, kuna magonjwa mengine yenye dalili kama hizo na ni daktari atakayekusaidia kutofautisha. Habari njema ni kwamba UTI inatibika kirahisi kwa antibiotiki, lakini unashauriwa kumuona daktari kabla ya kuzitumia kwani wakati mwingine kunywa maji mengi kunasaidia kusafisha njia ya mkojo. Unashauriwa kwenda haja ndogo mara unapojisikia kufanya hivyo, yaani kutobana mkojo kwa muda mrefu sana, kuhakikisha unajisafisha vizuri baada ya haja kubwa na baada ya kufanya ngono. |
Next
« Prev Post
« Prev Post
Previous
Next Post »
Next Post »
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
EmoticonEmoticon