Ndalichako ataja sababu za kuondoka NECTA tofauti na yanayosemwa


Waziri wa Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, amesema mfumo wa wastani wa alama za mtihani (GPA) haukuwa sabababu ya yeye kuondoka katika nafasi ya Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA).
Prof, Ndalichako alisema hayo wiki iliyopita wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari kutokana na uvumi uliozagaa mitaani ikiwemo kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kuwa alijiuzulu nafasi hiyo kutokana na kushinikizwa kuukubali mfumo huo.
Alisema aliondoka NECTA baada ya kufanya kazi katika baraza hilo kwa miaka tisa, hivyo muda huo aliona unatosha kwa yeye kuliongoza baraza hilo la mitihani nchini.
“GPA haikuniondoa NECTA kama ambavyo nimekuwa nikisikia maneno mitaani kuwa niliondoka ili kupisha mfumo huu wa GPA kuanza kutumiwa na baraza hili la mitihani nchini,”
Prof. Ndalichako alisema kuondoka kwake kulisukumwa na kazi kubwa alizokuwa amezifanya katika baraza hilo, pamoja na kuweka mifumo mbalimbali ya kisasa katika usajili na mambo mengine ya kitaalamu ambayo hayakuwapo kabla yake.
“Nimefika pale NECTA nikakuta kuna baadhi ya watendaji wanadai hawaejenda likizo kwa zaidi ya miaka mitatu, hii yote ilikuwa ni kutoka na mifumo iliyokuwa ikitumika ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa kwenye vichwa vya watu hivyo wao kama hawatakuwapo basi kazi nyingine hazifanyiki...nikamua kuanzisha mifumo ya kisasa na kuacha kutegemea vichwa vya watu,”
Prof. Ndalichako alisema sababu nyingine iliyomuondoa NECTA ni kutaka kujiendeleza kielimu kutoka alipokuwa wakati huo na kupanda katika ngazi nyingine, kwani kama angeendelea kubaki asingeweza kujiendeleza.
“Nilitoka Necta nikarudi Chuo Kikuu cha Dar es Salaamu ili kujiendeleza na hivi sasa mimi ni profesa lakini nilipokuwa Necta nilikuwa dokta, hivyo hayo maeneno yanayozagaa kuwa mimi nilikimbia GPA si ya kweli hata kidogo na mfumo huo ulianzishwa mimi nikiwa sipo pale,”
  NIPASHE
Previous
Next Post »