(Meneja
msaidizi wa kituo cha walemavu cha Usa River Rehabilitation
Centre,Sophia Moshi akibadilishana mawazo na meneja mkuu wa kituo
hicho,Claus Heim).
Mahmoud Ahmad, Arusha
SERIKALI imeombwa kuchukua hatua kali
kwa baadhi ya wazazi nchini wenye tabia ya kuwaficha watoto wao wenye ulemavu
hali ambayo imekuwa ikiwafanya wakose mahitaji ya msingi kama elimu na afya.
Ombi hilo limetolewa hivi karibuni na
uongozi wa chuo cha walemavu cha Usa River Rehabilitation Centre huku wakiiomba serikali iviangalie vituo vya
kulea watoto walemavu kwa kuvipatia ruzuku .
Akizungumza katika mahojiano maalumu
na gazeti hili chuoni hapo,meneja wa chuo hicho,Claus Heim alisema kwamba
serikali inapaswa kuhakikisha inawachukulia hatua kali za kisheria baadhi ya wazazi wenye tabia ya
kuwaficha watoto wao wenye ulemevu majumbani.
Alisema kwamba serikali inapaswa
kuweka sheria kali na kuhakikisha zinatekelezwa ili kuwapa fursa watoto wenye
ulemavu nchini kupata huduma za msingi kama elimu,afya,chakula pamoja malazi.
“Hawa wazazi wanaowaficha watoto
wenye ulemavu nchini je wanachukuliwa hatua gani?kila mtoto ana haki ya elimu
na afya lakini nani anawajibika”alihoji Heim ambaye ni raia wa nchini ujerumani
Hatahivyo,meneja msaidizi wa kituo
hicho,Sophia Moshi kwa upande wake alisema kwamba ni wajibu wa serikali
kuhakikisha inavipatia ruzuku vyuo vya ulemavu nchini ili viweze kujiendesha kwa kuwa vinakabiliwa na changamoto lukuki.
Alisema kwamba mtoto mwenye ulemavu
ana uwezo kama mtoto mwingine na hivyo kuitaka jamii kuwathamini watoto wenye
mahitaji maalumu badala ya kuwanyanyapaa.
Mbali na kauli hiyo Moshi alisema
kwamba chuo chao kimejipanga kujenga shule ya sekondari kwa lengo la kuongeza
mapato ya kuendesha chuo hicho badala ya kutegemea wafadhili ,kusajili kituo cha
afya kwa ajili ya matibabu ya mguu kifundo(club foot) sanjari na kusajili chuo
cha ufundi chuoni hapo.
Chuo hicho kilianzishwa mnamo mwaka
1988 na kinasimamiwa na kanisa la Kiinjili la Kilutheri(KKKT) Dayosisi ya Meru ,kwa sasa kina jumla ya wanafunzi 74 walemavu
ambao ni wasichana na wavulana ambapo nchi ya ujerumani ndiye mfadhili mkuu kwa
sasa.
EmoticonEmoticon