JK ateua Makamishna wa NEC.



JK ateua Makamishna wa NEC.

Zikiwa zimebaki siku 39 kufanyika uchaguzi mkuu, Rais Jakaya Kikwete amewateua Makamishna wawili wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Walioteuliwa kushika nyadhifa hizo ni Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mary Longway na Wakili wa Kujitegemea, Asina A. Omari.
Uteuzi huo ulioanza jana, umefanyika ikiwa ni siku 52 tangu amteue Mkurugenzi wa NEC, Ramadhan Kailima, Julai 25, mwaka huu.
Aidha, Rais Kikwete amewateua wakuu wawili wapya wa mikoa kujaza nafasi zilizoachwa wazi na wakuu wa mikoa ambao wanawania ubunge.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ilisema Rais Kikwete amemteua Amos Makalla, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Jordan Rugimbana, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Aidha, Rais Kikwete amewahamisha wakuu wawili wa mikoa, Mwantumu Mahiza, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga na Saidi Magalula, ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akitokea Mkoa wa Tanga.
Magalula anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Stella Manyanya, anayewania ubunge mkoani Ruvuma pia.
Makalla Mbunge aliyemaliza muda wake Jimbo la Mvomero na Naibu Waziri wa Maji, anachuku nafasi iliyoachwa wazi na Leonidas Gama, ambaye anawania ubunge mkoani Ruvuma.
Rugimbana ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Mahiza.
Taarifa ilisema uteuzi na uhamisho huo ulianza Septemba 12, mwaka huu na wakuu wapya wa mikoa wataapishwa kesho Ikulu, Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amemteua Victoria Richard Mwakasege, kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi.
Kabla ya uteuzi wake, Mwakasege alikuwa Naibu Balozi wa Tanzania nchini Burundi.
Aidha, Rais Kikwete amemteua Msaidizi wa Rais wa Diplomasia, Balozi Samwel Shelukindo, kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ilisema kuwa Rais Kikwete amemteua Zuhura Bundala, kuwa Balozi na Msaidizi wa Rais (Diplomasia) kujaza nafasi iliyoachwa na Shelukindo.
Kabla ya uteuzi wake, Bundala alikuwa Mkurugenzi Msaidizi na Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Afrika.
Taarifa hiyo ilisema vile vile kuwa Rais Kikwete amewateua wakurugenzi wengine wanne wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimatiafa na kuwapandisha cheo kuwa mabalozi.
Walioteuliwa ni Abdallah Kilima, ambaye anakuwa Balozi na Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati.
Kabla ya uteuzi wake, Kilima alikuwa Afisa Ubalozi Mkuu, Ubalozi wa Tanzania, Muscat, Oman.
Baraka Luvanda, ambaye anakuwa Balozi na Mkurugenzi wa Idara ya Sheria.
Kabla ya uteuzi wake, Luvanda alikuwa Mratibu wa Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu.
 Innocent Shiyo, ambaye anakuwa Balozi na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda.
Kabla ya uteuzi wake, Shiyo alikuwa Mkurugenzi Msaidizi katika Idara hiyo hiyo.
Anisa Mbega, ambaye ameteuliwa kuwa Balozi na Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora.
Kabla ya uteuzi wake, Mbega alikuwa Mkurugenzi Msaidizi, Ubalozi wa Tanzania, Kampala, Uganda.
Taarifa ilisema uteuzi huo wote ulianza jana.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete amemteua Dk. Tulia Ackson, kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanzia Septemba 9, mwaka huu.
Kabla ya uteuzi wake, Dk. Ackson alikuwa Mhadhiri wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Pia amemteua Mlingi Elisha Mkucha, kuwa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC).
Uteuzi huo ulianza Septemba 9, mwaka huu.
Taarifa ilisema Mkucha ni mwanasheria na mwajiriwa wa NDC kwa miaka 14 iliyopita, ambako ametumikia katika nafasi mbalimbali mpaka akawa Kaimu Mtendaji Mkuu.
Mkucha anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Gideon Nassari, aliyestaafu kwa mujibu wa sheria.
Vile vile, Rais Kikwete amemteua Profesa Muhammed Bakari Kambi, kuwa Mganga Mkuu wa Serikali.
Taarifa ilisema uteuzi huo ulianza tangu Septemba 9, mwaka huu.
Kabla ya uteuzi wake, Profesa Kambi alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tiba na Afya Shirikishi cha Muhimbili.
CHANZO: NIPASHE
Previous
Next Post »