PUBLIC NOTICE
BASATA LATAKA KUONDOLEWA/KUSITISHWA MARA MOJA KUCHEZWA KWA NYIMBO ZOTE ZENYE KUKENGEUKA MAADILI, SHERIA NA TARATIBU
Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) linawaagiza wasanii, wamiliki na waendeshaji
wa wavuti, tovuti na vyombo vya habari hususan radio na runinga kuondoa
na kuacha mara moja kurusha au kutangaza au kucheza nyimbo zote zenye
maudhui ya kashfa, matusi, kejeli, udhalilishaji ambazo zinahatarisha
kuigawa jamii ya kitanzania katika misingi yoyote hasa katika kipindi
hiki Taifa linapoendelea na kampeni za kisiasa na kujiandaa na uchaguzi
mkuu.
Kwa
mujibu wa kifungu namba 118 (a-d) cha Sheria ya Bunge namba 9 ya
Mawasiliano ya Mtandao ya mwaka 2010 ni marufuku kwa njia yoyote kwa mtu
au chombo chochote kutengeneza, kuzalisha, kusambaza au kutangaza
ujumbe ambao una mlengo wa matusi, dharau, uzushi au jinai kwa lengo la
kutukana, kutisha, kusumbua au kushusha hadhi ya mtu mwingine.
Aidha,
Sheria ya Bunge namba 4 ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 kifungu cha
45 (1) (a-c) kinatoa mamlaka kwa taasisi au mtu yeyote anayebaini
uvunjifu wa Sheria katika mitandao kutoa notisi kwa yeyote yule
anayesambaza au kutangaza ujumbe au maudhui yanayovunja sheria za nchi
kuacha mara moja au vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya
yeyote anayekaidi.
Ni
kwa msingi huu, BASATA linawaagiza wasanii, wamiliki wa wavuti, tovuti
na wale wenye akaunti kwenye mitandao ya kijamii kama sound cloud,
U-Tube, ITunes nk. kuondoa ndani ya siku saba (7) kuanzia siku ya kwanza
ya taarifa hii nyimbo zote zinazokengeuka maadili na kubeba mlengo wa
matusi, kashfa, kejeli na udhalilishaji wa watu wa kada mbalimbali
wakiwemo viongozi wa kisiasa na kitaifa.
Aidha,
BASATA linawakumbusha tena Wasanii wote nchini kuacha mara moja kubuni
na kutengeneza kazi za Sanaa zenye kuashiria kuigawa jamii katika
misingi yoyote ya kibaguzi na zaidi kutumia Sanaa kubomoa jamii badala
ya kuijenga.
BASATA
linawasisitiza wamiliki wa vyombo vya habari hususan radio na runinga
pia watangazaji na Ma DJs kuhakikisha hawawi chanzo cha kusambaza
maudhui yoyote ya Sanaa yenye mlengo wa kuibua chuki, matusi, kashfa na
mgawanyiko wa Taifa.
BASATA
kwa mamlaka yake chini ya Sheria namba 23 ya mwaka 1984 na yale ya
Sheria ya Mawasiliano ya Posta na Mitandao ya mwaka 2010 na ile ya
Makosa ya mitandao ya mwaka 2015 kwa kushirikiana na vyombo vya dola
halitasita kuchukua hatua kali za kisheria na kinidhamu kwa wasanii,
wamiliki wa wavuti, tovuti na vyombo vya habari ambavyo vitaendelea
kutangaza na kusambaza nyimbo zenye mwelekeo wa kuhatarisha usalama,
umoja na mshikamano wa Taifa.
BASATA
likiwa ni msimamizi na mratibu wa sekta ya Sanaa nchini linatambua
kwamba Sanaa ikitumiwa kwa ukengeufu inaweza kuwa chanzo kikuu cha
machafuko, mivurugano na kupotea kwa amani nchini. Hivyo umakini
unahitajika miongoni mwa wasanii katika kuzingatia weledi, maadili,
uzalendo kwa taifa na kuitumia Sanaa kama chombo cha kujenga jamii yenye
kuzingatia maadili.
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI, BASATA
EmoticonEmoticon