MBUNGE WA NCCR-MAGEUZI MOSES MACHALI AJIUNGA NA CHAMA CHA ACT WAZALENDO MWAKA HUU MNAHAMA KWELI.


KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, leo ataongoza mapokezi makubwa ya Mbunge wa Kasulu Mjini, mkoani Kigoma, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), ambaye atatambulisha rasmi kuwa mwanachama wa ACT- Wazalendo.
 

Machali ataambatana na Madiwani wawili, Kamishna wa Mkoa mmoja, Katibu wake, Wenyeviti na Makatibu wa kata 12 zilizo kwenye Jimbo la Kasulu Mjini.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na ACT-Wazalendo, ilisema katika mapokezi hayo, Kabwe pia atawapokea Makatibu Uenezi tisa wa jimbo hilo lenye jumla ya kata 15 za uchaguzi.

Mbali na viongozi hao, wengine ambao wataambatana na Machali kujiunga ACT-Wazalendo ni Wenyeviti 101 wa Matawi na Makatibu 98 na wanachama 648 wote kutoka NCCR-Mageuzi, jimboni humo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya mapokezi hayo, Bw. Kabwe atakwenda mkoani Shinyanga kuwapokea viongozi, madiwani kutoka vyama mbalimbali Julai 25, mwaka huu.

Julai 26, mwaka huu, Kabwe atakutana na watia azma wa nafasi ya ubunge katika majimbo ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuweka mikakati ya ushindi wa kishindo.

Wakati Kabwe akiwa mkoani kwa ajili ya kuwapokea wanachama wapya, jijini Dar es Salaam Julai 22, mwaka huu, viongozi wengine watakuwa na jukumu la kuwapokea wanachama na waliokuwa madiwani katika vyama tofauti vya siasa nchini.
Previous
Next Post »