MAUAJI YA KISHIRIKINA YAUMBUA SERIKALI




Baada ya albino, nani?
• Mwito wa elimu, mabadiliko
Na Ndimara Tegambwage
SIYO siri tena. Katika Tanzania, baadhi ya wananchi wanawinda wananchi wenzao wenye ulemavu wa ngozi – Albino – na kuwaua.
Mauaji yanaenda sambamba na uvumi kwamba viungo vya albino ni mali na kwamba aliyenavyo aweza kupewa dawa ya kumwezesha kuwa tajiri.
Hivi sasa mbio za kupata utajiri zimechukua kasi ileile ya mauaji. Wengi wanatamani utajiri wa miujiza. Kadri fikra hizo zinavyozingatiwa, ndivyo albino wanavyoendelea kuangamia.
Wanawaua. Wanakata viungo vyao na kuvipeleka kwa watu masikini lakini wenye imani ya kuwapa utajiri watu wengine. Hata makaburi ya albino yanafukuliwa ili kupata viungo. Wazimu!
Mauaji ya albino ni mauaji sawa na yale ya mtu yeyote. Ni uhalifu usiosameheka. Ni msiba mkubwa na endelevu wa kitaifa.
Lakini madhara makuu ni kwamba mauaji haya yana tabia ya kuambukiza. Leo vinatakiwa viungo vya albino, kesho vitatakiwa vya nani?
Haitakuwa rahisi kujua albino wote waliouawa na waliosalia, kwani hakuna takwimu za idadi ya albino nchi nzima. Idadi ya waliouawa ni ya kuokoteza hapa na pale au ile iliyoripotiwa na waandishi wa habari za uchunguzi.
Hii ni kutokana na sababu zifuatazo:
Kwanza, kuna wanaoishi mbali na miji na taarifa juu yao hazipatikani kwa urahisi au hazipatikani kabisa.
Pili, kuna wale ambao wazazi wao walishiriki kuwaua kutokana na imani kwamba kuzaa albino ni “balaa.” Wazazi hawatasema au watasingizia sababu nyingine za kifo.
Tatu, kuna wanaoogopa kusema matukio hayo kutokana na kutishiwa au hata kuhongwa fedha au ahadi ili wakae kimya. Kimya hiki, katika maeneo haya, kinaweza kuwa kinaendeleza mauaji mengi zaidi ya albino.
Bali kuna jambo moja ambalo limefahamika. Katika siku za karibuni, kila albino aliyeuawa imedaiwa ni kwa sababu ya kupata viungo vya mwili wake ili vipelekwe kwa “mganga” kutengenezea “dawa ya utajiri.” Utajiri umekuwa ni pamoja na vyeo vya kisiasa na madaraka serikalini.
Bila shaka idadi ya albino, haiwezi kutosheleza mahitaji ya wanaotaka utajiri au vyeo vya siasa. Hata hivyo, hakuna anayeua albino mmoja na kumweka nyumbani kusubiri mteja anayehitaji kiungo fulani.
Hata kama kuna mwenye ghala la waliouawa, hakuna anayejua ni kiungo kipi mganga fulani atahitaji na kama atataka kilichokauka au kibichi.
Kwa hiyo albino waweza kuisha. Lakini pia waganga waweza kusema albino “si mali tena;” wakataja mtu mwingine wa jinsia, cheo, umaarufu na nafasi fulani katika jamii.
Hapo ndipo itakuwa mshikemshike, na labda ndipo watawala watakurupushwa usingizini na kuonekana wamekuwa wakilea mauaji endelevu.
Kama awali mahitaji yalikuwa kiungo chochote cha albino yeyote; fikiria idadi ya watakaouawa pale waganga wakianza kusema wanataka kiganja cha mkono wa kulia wa kichanga cha siku 10. Vichanga vingapi vitauawa?
Mahitaji ya viungo vya binadamu yaweza kwenda yanapanuka kila siku. Chukua mfano wa waganga watakaotaka kichwa cha bibi kizee wa miaka 80; pua ya mtoto wa kike wa mwenyekiti wa mtaa; au magoti yote mawili ya mama yake diwani.
Kasheshe itaaanza kukomaa pale utakaposikia sasa waganga wanataka nyama ya katikati ya mgongo ya mama mkwe wa mkurugenzi wa halmashauri; huku wengine wakidai matiti yote mawili ya binti wa mkuu wa wilaya na wengine wakitaka visigino vyote vya mke wa mbunge.
Labda baada ya hapo serikali inaweza kustuka, kwamba hali inaanza kuwa mbaya na kukumbuka kuwa laiti ingechukua hatua wakati albino wanapiga yowe.
Hapo ndipo kimbunga cha aina yake kinaweza kutokea. Leo utasikia mganga anataka masikio mawili ya dada yake (wa kuzaliwa) mkuu wa mkoa. Kesho utasikia mganga mwingine anataka kiganja cha mkono wa kushoto cha mtoto wa kiume wa waziri.
Yote hayo ni nyongeza tu kwa taarifa za awali, kwamba mganga mwingine anataka titi la kushoto la mama mkwe wa waziri mkuu.
Wakati waziri mkuu wa zamani anaanza kuchekelea kuwa afadhali yeye hayuko tena kwenye uongozi, zinaingia zile motomoto kwamba mganga anataka utumbo mdogo wa aliyewahi kuwa waziri mkuu.
Waganga hawana simile. Kadri idadi ya wanaosaka utajiri na hata vyeo katika siasa inavyoongezeka, nao wanapanua wigo wa matakwa ya dawa.
Mara hii habari zitasambaa kuwa kwa utajiri mkubwa sharti upeleke figo za rais mstaafu. Uuuhwi! Hapa marais wastaafu watawindwa kama swala, wakati walioukosa wakichekea kiganjani.
Kwa utajiri wa juu zaidi ya hapo, sharti lipatikane taya zima la chini la rais aliyeko kitini. Ni kazi kubwa kulipata kutokana na ulinzi mkali alionao lakini nani anajua kiasi ambacho mganga anatarajia kutoza mteja wake?
Kama hatua ya kulegeza mahitaji, taarifa zitasambazwa kwamba kwa utajiri na vyeo vya kati, waganga wanataka shingo la waliowahi kuwa viongozi wakuu visiwani.
Baada ya miezi kadhaa taarifa zitaenea kuwa kwa biashara nzuri na nchi za nje, inahitajika ngozi ya waziri kiongozi au utumbo mkubwa wa mkurugenzi wa ikulu.
Sasa woga utakuwa umetanda. Wananchi watakuwa wanapumua mapigo nusunusu. Watawala watakuwa wamekuwa sehemu ya ushirikina katika kujaribu kujikinga.
Kama kwamba matakwa ya waganga yatakuwa yameanza kuzoeleka, ndipo utasikia sasa wanataka uti wa mgongo wa kiongozi wa chama cha kikuu cha upinzani.
Baada ya siku kadhaa utasikia wanataka ubongo wa kardinali na kabla wananchi hawajaanza kutafakari vema matakwa hayo, watasikia sasa waganga wanataka ulimi wa sheikh mkuu.
Huku hoja nzito zikiwa zimepamba moto bungeni, utasikia waganga sasa wanataka kilo mbili za nyama ya paja la kulia la wabunge machachari (na majina yao yanatajwa).
Ni hofu kuu. Spika wa bunge anajitahidi kuyeyusha kile anachoita uvumi lakini siku inayofuata taarifa zinafika kwamba waganga sasa wanataka ubavu mzima (kidali) wa spika.
Na bado watu wengi wanakwenda kwa waganga. Hapa ndipo wengi wanakumbana na kisiki. Waganga wanataka korodani za watuhumiwa wa ufisadi. Eh!
Utawala unayumba. Majeshi yanawekwa kwenye hali ya tahadhari. Lakini katikati ya maandalizi zinakuja taarifa kwamba waganga wanataka moyo wa mke wa mkuu wa majeshi.
Polisi wanapoanza doria, taarifa zinamiminika kuwa waganga sasa wanataka macho yote mawili ya binti mkubwa wa mkuu wa jeshi la polisi.
Huku upelelezi ukiwa unaendelea kujaribu kuona kilicholeta janga, taarifa zinaingia kwamba waganga sasa wanataka mikono yote miwili ya mkuu wa mashushushu.
Kana kwamba waganga sasa ndio wanatawala, taarifa zinaenea kote, bara na visiwani, kwamba waganga wanataka koromeo za waandishi wa habari “kaidi.”
Hivyo ndivyo itakavyokuwa, iwapo watawala hawatasitisha mauaji ya albino.
Vita vya kusitisha mauaji ya albino ni vita vya kuzuia maafa makubwa zaidi kwa jamii nzima.
Silaha kuu ni elimu. Darasani na mitaani; kwenye mikutano ya hadhara, vijiweni, maofisini na viwandani, ujumbe uwe mmoja:
“Albino ni mtu kama wewe na mimi. Ana haki ya kuishi. Hakuna mwenye viungo vya kuzalisha utajiri.”
Mauaji ya albino yafafanuliwe kuwa ni ukatili. Ni uhalifu mkuu. Ni ukiukwaji wa haki za binadamu. Kunyamazia haya, au kutoyakomesha ni kujiunga na wauaji.
Elimu inaweza kuimarishwa kwa sheria, taratibu, kanuni na ufuatiliaji usiokoma na kwa njia hii, mabadiliko yaweza kutokea. Bali sharti idadi ya albino nchini ifahamike; kuwepo utaratibu wa kudumu wa kujua wanaozaliwa, wanaofariki na kwa sababu zipi.
Ukatili, ujinga, ushirikina, uzembe na dharau si maadili ya jamii nyofu wala watawala. Kushindwa kulinda maisha ya albino mmoja ni kukiri kushindwa kulinda maisha ya jamii nzima. Albino wasiuawe.
Simu:0713 614872
Imeili:ndimara@yahoo.com
Blogu: Uhuru Hauna Kikomo...
Previous
Next Post »