Na Martin Malera
MBUNGE wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM),
ameliomba Bunge kubadilisha kanuni ili Waziri wa Kilimo na Chakula, Mhandisi
Christopher Chiza, achapwe viboko bungeni akamuonyeshe mkewe.
Filikunjombe, alisema kanuni hiyo iruhusu
mawaziri wote wanaoshindwa kujibu maswali ya wabunge kwa ufasaha, wachapwe
viboko na kutolea mfano wa Waziri Chiza kwamba, alipaswa kuchapwa viboko kwa
kushindwa kujibu swali la Mbunge wa Mwibara, Kange Ligola (CCM), juzi.
Akiomba mwongozo wa Spika jana bungeni baada ya
kipindi cha maswali na majibu, Filikunjombe, alisema Waziri Chiza mwenye
dhamana ya kilimo, jana alishindwa kujibu swali la Ligola na badala yake
aliishia kutoa maneno ya kejeli kwa Mbunge huyo.
“Jana wakati wa kipindi cha maswali na majibu,
Waziri Chiza alishindwa kabisa kujibu swali la Ligola aliyetaka Serikali kutoa
kauli juu ya mazao ya wakulima yaliyonunuliwa kwa mkopo na yale ambayo
hajanunuliwa na yako kwenye hatari ya kuharibika wakati wa msimu wa mvua…
“Badala ya kujibu swali hili, Mheshimiwa Waziri
aliishia kutoa maneno ya kejeli kwa Ligola kwamba yeye anayeshindwa kuelewa
ndiye mzigo…
“Mwalimu Nyerere alisema wakati wa utawala wao
hawakuwa na mswalia mtume kwa wala rushwa, maana hawakumuachia hakimu kuhukumu,
kwani walikuwa wanawachapa viboko sita wakati wa kuingia na sita wakati wa
kutoka wakawaonyeshe wake zao.
“Na sisi tusiwe na mswalia mtume kwa mawaziri
wanaoshindwa kujibu maswali ya wabunge, tuwachape viboko bungeni wakawaonyeshe
wake zao,” alisema Filikunjombe na kuibua vicheko kwa wabunge ukumbini hapo,
akiwemo Chiza mwenyewe.
Katika swali lake la nyongeza juzi, Ligola
alisema Waziri Chiza ni mzigo, kwani ameshindwa kuwasaidia wakulima wa mahindi,
mpunga, pamba na mazao mengine ambao hawana uhakika wa soko na mazao yao
yanaozea kwenye maghala.
Alisema katika jimbo lake la Mwibara, baadhi ya
wakulima wa mahindi mazao yao yamekopwa na haijulikani watalipwa lini huku
mazao mengine yakikosa soko.
Akijibu swali hilo kwa jazba, Chiza alisema yeye
sio mzigo bali Mbunge huyo ndiye mzigo kutokana na uelewa wake mdogo.
EmoticonEmoticon