TAARIFA ZA AWALI KUHUSU BASI LA JAPANESE KUTUMBUKIA MTONI MKOANI NJOMBE

Abiria kadhaa waliokuwa wakisafiri na basi la kampuni ya japanese aina ya Yutong kutoka Ikonda wilayani Makete kwenda Makambako, wamenusurika kifo huku wengine wakijeruhiwa baada ya basi hilo kutumbukia mtoni.

Ajali hiyo mbaya imetokea kwenye daraja lililopo eneo la Mpandu wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe jana majira ya saa 9 mchana. 
Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo wamedai kuwa imesababishwa na basi hilo lenye namba za usajili T 261 CMK kushindwa kupanda mlima kulikosababishwa na gia kufeli hali iliyopelekea basi hilo kuanza kurudi nyuma kwa kasi hadi kutumbukia mtoni. 

Kufuatia ajali hiyo baadhi ya magari yaliyokuwa yakipita eneo hilo yalikuwa yakitoa msaada kwa manusura wa ajali hiyo huku majeruhi wakikimbizwa hospitali ya Kibena mkoani Njombe kwa ajili ya matibabu. 
 Sista wa kanisa katoliki akiendelea kuugulia maumivu baada ya kunusurika kwenye ajali hiyo
 Mashuhuda wa ajali hiyo
 Abiria wakipanda basi jingine ili waendelee na safari
Mwandishi wa eddy Blog aliyefika eneo la tukio ameshuhudia baadhi ya abiria walionusurika wakipanda kwenye basi lingine la kampuni hiyo ili kuendelea na safari. 

Mmoja wa abiria hao aliyejitambulisha kwa jina la mama Imma amesema haelewi ni nini kilichotokea lakini alishangaa kushtushwa na kishindo cha kuanguka kwa basi hilo ila anamshukuru Mungu kutoka salama katika ajali hiyo. 
Basi lilipata hitilafu pale juu kabla ya kuanza kurudi nyuma kwa kasi.
Hadi mwandishi wetu anaondoka eneo la tukio majira ya saa 11 jioni majeruhi wote walikuwa wamepelekwa hospitalini na abiria wengine kuendelea na safari na polisi walikuwa hawajafika eneo la tukio, hivyo bado hatujapata uhakika ni abiria wangapi wamejeruhiwa ama pengine kumetokea kifo

CREDIT TO EDDY BLOG
Previous
Next Post »