VIONGOZI WA DINI WAJERUHIWA BAADA YA KURUSHIWA BOMU JIJINI ARUSHA


TAFRANI kubwa imeukumba mtaa wa Majengo jijini Arusha, baada kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu kulipuka kwa kishindo na kuwajeruhi wawili akiwamo Ustadh mmoja na mgeni wake kutoka Nairobi nchini Kenya.

Tukio hilo lililotokea usiku wa Alhamisi Julai 3, 2014 na kuthibitishwa na polisi limeibua tahauki kwa wakazi wa Arusha na kusababisha waumini wa dini ya Kiislamu kushindwa kufanya ibada ya sala ya Alfajiri leo Ijumaa.

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha Liberatus Sabas, amesema  kuwa tukio hilo lilitokea jana saa 11:15 usiku nyumbani kwa, Ustadhi Sudi Ali Suli, wakati wakila daku na mgeni wake kutoka Nairobi nchini Kenya, Mhaji Hussein.

Wakiongea na mwandishi, baadhi ya wananchi katika eneo hilo wamesema baada ya kupata taarifa ya kutokea kwa tukio hilo waliingiwa na hofu na kuwafanya baadhi yao kushindwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kufanya swala ya alfajiri. Kamanda Sabas alisema Ustadh Sudi na mgeni wake aliyefikia nyumbani kwake walijeruhiwa katika tukio hilo.

“Wakati bado wakiendelea kupata chakula walisikia kishindo kikubwa ambacho kilipasua kiyoo cha dirisha na bomu hilo likarushwa ndani na kusababisha mlipuko mkubwa uliowajeruhi miguuni lakini kwa bahati nzuri hakujatokea kifo katika tukio hili,”alisema Sabas.

Amesema kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa bomu hilo limetengenezewa kiwandani, na kuwa mtu aliyetekeleza tukio hilo alikimbilia kusiko julikana usiku huo baada ya kulitupa ndani ya nyumba hiyo na kuwa majeruhi wamejeruhiwa vibaya sehemu za miguuni.

Amesema Jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kuweza kubaini kama kuna kundi la watu au mtu mmoja aliyehusika na kuwa majeruhi hao wanapata matibabu katika Hospitali ya mkoa huo ya Mount Meru.

Credit: Fikrapevu
Previous
Next Post »