MITAMBO YA IPTL KUANZA KUZALISHA MEGAWATI 100 ZA UMEME

·        IPTL kuongeza uzalishaji hadi megawati 200 mwakani
·        Kushusha zaidi bei ya umeme hadi chini ya senti nane za marekani

UZALISHAJI umeme katika kampuni ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) umefikia megawati 100 ambayo ni kiwango cha juu cha uwezo wa mitambo yake, kiwango kilichofikiwa tarehe 15 Juni, huku uongozi wa kampuni hiyo wakiahidi kutekeleza mipango mkakati yake yote ya utanuzi kwa awamu.  

Hayo yalibainishwa na Katibu na Mwanasheria Mkuu wa IPTL/Pan African Power Solutions (PAP), Bw. Joseph Makandege alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa ahadi za viongozi wa kampuni hiyo kwa umma na mamlaka za serikali tangu PAP iliponunua IPTL.

“Tarehe 15 mwezi wa sita mwaka huu, mitambo ya IPTL iliyopo eneo la Tegeta, ilianza kuzalisha megawati 100 za umeme, ambazo ndiyo uwezo wa mitambo hiyo. Hii ni moja ya ahadi zilizotolewa na uongozi wa PAP wakati wa ununuzi wa mitambo ya IPTL,” alisema Makandege .

Alisema IPTL ambayo inamilikiwa na kampuni ya kizalendo ya Pan African Power Solutions Tanzania Limited, inaendelea na jitihada zake za kutimiza ahadi yake ya kuwapunguzia wateja/walaji adha ya gharama ya umeme Tanzania.

“Tumepanga kuzalisha megawati 200 kwa kutumia mitambo inayoendeshwa kwa kutumia gesi ifikapo Desemba 2015, ambapo tutauza umeme wake kwa chini ya dola nane za kimarekani, ikiwa ni awamu ya kwanza ya utanuzi. Katika awamu ya pili ya utanuzi, tumepanga kuzalisha megawati 300 ifikapo Desemba 2017.

“Tuliahidi kupunguza bei zetu, kuongeza uzalishaji mpaka kufikia kiwango cha juu cha mitambo yetu na kuendelea kutanua mitambo yetu ili kuweza kuzalisha megawati 500 baada ya kibadilisha mfumo yake iweze kutumia gesi. Hatua hii itawezesha IPTL kupunguza zaidi bei zake hadi kufikia kati ya senti sita na nane za kimarekani kwa kila unit. Ndani ya kipindi hiki kifupi, tumeweza kudhihirisha uwezo wetu wa kutimiza ahadi zetu zote,” alisema Bw. Makandege.
Previous
Next Post »