WANAOUZA VYETI VYA KUZALIWA KUKIONA!


SERIKALI imetangaza kuwachukulia hatua kali wote watakaobainika kuuza vyeti vya kuzaliwa kwa bei kubwa kinyume cha sheria.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki, alipojibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Pauline Gekul (CHADEMA).
Mbunge huyo alitaka kuelezwa iwapo ni sahihi vyeti vya kuzaliwa kuuzwa sh 15,000 kama inavyofanyika.
Alitaka kuelezwa kwanini vyeti hivyo havipatikani ngazi ya mitaa ili kuondosha usumbufu unaojitokeza wa kufuata vyeti hivyo kwenye vituo vya afya.
Katika swali la msingi, mbunge huyo pia alitaka kuelezwa gharama anayopaswa kulipa Mtanzania pale anapohitaji cheti cha kuzaliwa.
Akijibu swali hilo, naibu waziri huyo alisema ni makosa kwa mtu kuuza cheti cha kuzaliwa zaidi ya sh 15,000.
Alisema cheti cha kuzaliwa hutolewa chini ya sheria ya uandikishaji wa vizazi na vifo sera ya 108.
“Sheria hii kupitia tangazo la serikali namba 245 la Julai, 2000 imeanzisha gharama za uandikishaji na utoaji wa cheti cha kuzaliwa.
“Gharama hizo zinatofautiana na aina ya kizazi kinachohitaji kusajiliwa na muda wa kusajili kama ifuatavyo.
“Kwa mtoto mwombaji ambaye ameandikishwa ndani ya siku 90 tangu kuzaliwa ni sh 3,500; kwa mtoto mwombaji aliyechelewa kuandikishwa yaani baada ya siku 90 tangu azaliwe, lakini chini ya miaka 10 gharama ni sh 4,000 na kwa usajili wa mwombaji aliye na umri wa zaidi ya miaka 10 tangu kuzaliwa gharama ni sh 10,000,” alisema Angela
TZ-DAIMA
Previous
Next Post »