MAONESHO YA WAJASIRIAMALI KUFANYIKA KIGALI NOVEMBA

Wajasiriamali wamehimizwa kujiandikisha kwa wingi ili waweze kushiriki katika maonesho ya 15 ya wajasiriamali ya sekta isiyo rasmi yanayoshirikisha nchi za  Jumuiya ya Afrika Mashariki yajulikanayo kama Nguvu ya kazi/Jua kali yanayotarajiwa kufanyika November 30 hadi desemba 7, 2014 mjini Kigali Rwanda.
Wito huo umetolewa na Afisa Habari Mkuu wa Wizara ya Kazi na Ajira,  Ridhiwani Wema alipokuwa akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam na kusema kwamba lengo la kuwahimiza wajasirimali kuweza kujitangaza nje ya nchi na kupanua wigo wa soko la bidhaa zao linadhamiria kuongeza ajira.
“naowaomba wajasiriamali waweze kujitokeza kwa wingi ili kujiandikisha na hivyo kuweza kushiriki maonesho haya ambayo yatajumuisha nchi za Afrika Mashariki na hivyo kuwapa fursa ya kupanua wigo wa soko kwa bidhaa zinaotengenezwa na wajasiriamali hao,” alisema Ridhiwani.
Aliongeza kuwa  maonesho hayo yana malengo ya kuongeza fursa za ajira kupitia uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, kuchochea ubunifu, kupanua wigo wa masoko na kuwaunganisha wajasiriamali wadogo katika ngazi ya nchi na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Aidha alisisitiza  kuwa ili mjasiriamali aweze kushiriki katika maonesho hayo ni lazima awe mzalishaji wa bidhaa inayohitajika katika maonesho, pia bidhaa hizo ziwe zenye ubora  kwa kukubalika na  ubora wa viwango (TBS) na viwango vya taasisi inayosimamia vyakula dawa,TFDA, kadhalika anuani ya kudumu ya mahali anapofanyia kazi mjasiriamali husika.
Naye   Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wajasiriamali Tanzania, Joseph Rweyemamu aliongeza kuwa kuna umuhimu sana kwa wajasiriamali kushiriki maonesho haya kwa sababu ni njia mojawapo ya kujitangaza nje ya nchi kutokana na  bidhaa zao.
Maonesho hayo yalianzishwa  mwaka 1999 jijini Arusha, wakati wa kusainiwa kwa mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,  na yamekuwa yakiendelea kufanyika kila mwaka kwa kuzunguka nchi zote za Afrika Mashariki, ambapo kwa Tanzania bara yalifanyika mwaka 1999,2006 na 2009.
Previous
Next Post »