Usajili wa Domayo waivuruga TFF

Frank Domayo ‘Chumvi’



SIKU moja baada ya uongozi wa Azam FC kunyaka saini ya aliyekuwa kiungo wa Yanga, Frank Domayo ‘Chumvi’ akiwa kambini Tukuyu, Mbeya, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, amemteua Wakili Wilson Ogunde kuchunguza mlolongo mzima wa tukio hilo.
Domayo alisajiliwa juzi ikiwa ni siku chache baada ya Azam kumnasa nyota mwingine wa Yanga, Mrundi Didier Kavumbagu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Malinzi alisema kambi ya taifa ina miiko yake na hiyo ndiyo sababu kubwa iliyomfanya kumteua wakili huyo kwenda kuchunguza sakata hilo.
Alisema ameamua kumteua Ogunde, ili akija kutoa majibu ya tukio hilo asiwepo mtu wa kulalamika juu ya maamuzi hayo, kwani wakili atajua suala hilo liko katika kanuni za maadili au usajili na hapo ndipo TFF itatoa uamuzi.
Malinzi alisema wakili huyo amepewa siku 14 ili kurejesha taarifa rasmi juu ya tukio hilo na watalifanyia kazi bila ya kupendelea wala kumuogopa mtu yeyote.
“Kama ikigundulika kuna kanuni imekiukwa, tutachukua hatua bila ya kutazama sura wala kuangalia mtu na hatutapendelea mtu yeyote,” alisema Malinzi.
Alisema wao TFF hawawezi kumnyima riziki mchezaji yeyote, ila cha muhimu ni kufuata sheria na kudai kuwa hili lote linachangiwa na wachezaji kutokuwa na wasimamizi wao.
Malinzi alisema kuwa kwa sasa watakuwa makini kuangalia usajili wa wachezaji, kwani hakuna mchezaji huru hasa kwa hawa vijana wanaochipukia kwa sasa, kwani kuna watu waliowalea hadi kufikia hatua hii waliyofikia sasa.
Katika hatua nyingine, Malinzi alisema kesho Kamati ya Utendaji ya TFF inatarajiwa kukutana, na miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa itakuwa ni muundo wa Ligi Kuu na kudai kuwa Kamati ya Mashindano itapewa nafasi ya kuwasilisha mapendekezo.
Malinzi aliyasema hayo baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa ligi msimu ujao inatakiwa kuwa na timu 16 huku habari nyingine zikidai kuwa kuna harakati za kurejeshwa kwa timu ya Ashanti United iliyoshuka daraja.
Previous
Next Post »