MFANYAKAZI WA IKULU AFIA UWANJANI JANA KATIKA SHEREHE ZA MEI MOSI



Watu tisa waanguka na kupoteza fahamu maadhimisho ya Mei mosi



MAADHIMISHO ya sherehe za Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) ambayo kitaifa yalifanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam jana, yameingia dosari baada ya ofisa wa Ikulu, Rashid John Chilwangwe kufariki dunia akiwa katika maadhimisho hayo.
Chilwangwe alipatwa na tukio hilo majira ya saa nne asubuhi, nje ya Uwanja wa Uhuru akiwa anasubiri kuingia na maandamano yaliyokuwa yakipita uwanjani mbele ya Rais Jakaya Kikwete, yakitokea viwanja vya Mnazi Mmoja.
Walioshuhudia tukio hilo, waliliambia gazeti hili kuwa Chilwangwe ambaye anafanya kazi katika moja ya idara za Ikulu jijini Dar es Salaam, alianguka ghafla na kisha kubebwa na wafanyafakazi wa Chama cha Msalaba Mwekundu na kuhifadhiwa kwenye moja ya mahema yaliyoandaliwa uwanjani hapo kwa ajli ya huduma za dharura.
Akiwa ndani ya hema hilo, baadhi ya madaktari walijitahidi kutoa huduma ya kwanza ya matibabu, lakini hata hivyo wakati akiendelea kupata matibabu alifariki dunia.
Haikuweza kujulikana sababu hasa ya kifo cha ofisa huyo wa Ikulu kwani madaktari waliokuwapo eneo hilo hawakuwa tayari kuzungumzia kwa kina tukio hilo la kusikitisha.
Kamanda wa Polisi  Mkoa wa kipolisi Temeke, Englibert Kiondo, alikiri kutokea kwa tukio hilo ambalo alisema limetokana na Chilwangwe kusumbuliwa na ugonjwa wa moyo na kisukari.
Kiondo alisema kuwa kifo hicho kilichangiwa na mwendo mrefu aliotembea na kusababisha kuamsha maradhi yake ya moyo na kisukari, na hivyo kupoteza nguvu na kuanguka ghafla hatimaye kupoteza maisha.
Kiondo alisema kuwa baada ya kufariki, mwili wake ulipelekwa katika hospitali ya Wilaya ya Temeke kwa uchunguzi zaidi.
Mbali na tukio hilo, pia Tanzania Daima ilishuhudia uwanjani hapo watu tisa wakiishiwa nguvu na kuanguka kutokana na matatizo mbalimbali ya kiafya.
Tanzania Daima lilipomfuata mganga mmoja wa Manispa ya Temeke aliyegoma kutaja jina lake, aliyekuwa akiwahudumia wagonjwa hao katika hospitali ya uwanjani hapo, alisema chanzo cha kuanguka kimetokana na baadhi yao  kufika uwanjani hapo bila kula.
Mganga huyo alifafanua kuwa wapo watu wanne ambao walianguka kutokana na ukosefu wa sukari mwilini.
Alisema watu watatu waligundulika kuwa na shinikizo la damu huku wengine wawili wakisumbuliwa na malaria, hata hivyo watu hao walipatiwa tiba na kuruhusiwa kurudi majumbani kwao.

Previous
Next Post »