Kondo la nyuma linapoliwa, kutengeneza dawa, vipodozi


Ni kama sahani ya kwanza ya mlo kwa mtu yeyote kabla hajazaliwa. Ni eneo la kwanza lenye manufaa  kwa viumbe wengi wakiwa bado hawajauona ulimwengu.
Kwa binadamu, sahani hii ni ya muda usiozidi miezi tisa na baada ya hapo kazi yake huwa imekwisha, hivyo kuondolewa.
Hili ni kondo la nyuma,  kwa lugha ya Kiingereza huitwa placenta. Huwa ni sehemu ya mwili wa mama anapokuwa mjamzito. Sehemu hiyo humsaidia mtoto kupata chakula na hewa kutoka kwa mama akiwa tumboni.
Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani ya mwili, Meshack Shimwela anasema kondo la nyuma ni ogani iliyojishikilia katika ukuta wa nyumba ya uzazi ambayo huunganika na kitovu cha mama  na  hivyo kuwa kama daraja linalomuunganisha mama na mtoto kabla hajazaliwa.
Ogani hii husafirisha hewa safi, damu, huchuja chakula na kukitoa kwa mama kwenda kwa mtoto, hutoa hewa chafu pia na uchafu kutoka kwa mtoto kwenda nje.
 “Kondo la nyuma si nyumba ya uzazi bali ni kiungo kinachoumbwa mara baada ya mimba kutungwa kwa sababu ya kumuunganisha mama na mtoto,” anasema Dk Shimwela.
Baada ya mtoto kuzaliwa kiungo hicho hutoka mwilini mwa mama anaposukuma mtoto au hutolewa na madaktari  anapofanya upasuaji.
Pamoja na kumsaidia mtoto kupumua, ogani hiyo humlinda mtoto na maambukizi ya magonjwa iwapo yapo kwenye mwili wa mama na huzalisha vichocheo vinavyoulinda ujauzito.
Baada ya mama kujifungua tu, kondo la nyuma huishia hapo hapo na kutupwa. Lakini si wote wanaolitupa; hulitumia kama dawa.
Baadhi hulikaanga na kula kama nyama, wengine kukausha na kutengeneza tembe au vidonge na pia wapo wanaolila likiwa bichi hivyo hivyo mara tu  baada ya kutoka tumboni mwa mama.
Nchini China na Vietnam, hii hufanywa kama mila kwa kondo la nyuma  kuandaliwa na kuwa chakula cha mama.
Makabila ya mataifa haya yanaamini kuwa kondo la nyuma lina utajiri wa viinilishe mbalimbali ambavyo mama huhitaji mwilini ili apone kwa haraka baada ya kujifungua.
Previous
Next Post »