Simanzi na vilio jana vilitawala katika Mtaa wa Kijitonyama Mpakani A, baada ya watoto watatu wa familia jirani kufariki dunia baada ya kuzama katika bwawa la kuogelea walipokuwa wakisherehekea siku ya kuzaliwa mtoto mwenzao aliyetimiza mwaka mmoja.
Tukio hilo lilitokea juzi jioni katika Hoteli ya Landmark, Kunduchi Beach Dar es Salaam.
Waliofariki katika ajali hiyo ni Ndimbumi Sisala (9), mwanafunzi wa darasa la nne Shule ya Msingi Kijitonyama, Janeth Kihoko (9) wa darasa la nne Shule ya Msingi Dk Omar Ali Juma na Eva Mwakatobe (11) aliyekuwa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Shekilango.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 11:00 jioni.
Tukio lilivyokuwa
Watoto hao walichukuliwa na jirani yao, Anita Mboka kwenda kusherehekea nao siku ya kuzaliwa kwa mtoto wake, Derick Mboka.
Walioshuhudia tukio hilo walisema kuwa baada ya kufika hotelini hapo, watoto walianza kucheza mpira na wengine kuogelea huku mama aliyewapeleka pamoja na wale vijana wakiwa wamekaa wakipata vinywaji.
Kaka wa marehemu Janeth, Goodluck Kihoko (14) alisema yeye na watoto wenzake zaidi ya 20 waliondoka Kijitonyama wakiwa na vijana wanne kwenda kwenye sherehe hiyo.
“Tuliondoka hapa saa kumi na moja jioni, baada ya kufika kule tulianza kuogelea kwenye bwawa, watoto wengine walikuwa wanakwenda kuogelea kwenye maji marefu, walizuiliwa mara tatu, lakini baada ya walinzi kuondoka walirudi na kuzama,” alisema.
Alisema waliona mwili wa Janeth ukielea juu ya maji na kuwaita walinzi ambao waliwapuuza, baada ya muda wakafika na kuona mwili wa pili ukiibuka.
“Tuliwaita walinzi sana, ndipo wakafika na wakati huo mama na wale vijana walikuwa mbali na pale tulipokuwa tukiogelea,” alisema Goodluck.
Mboka hakupatikana baada ya kujifungia nyumbani kwake na majirani walisema ni kutokana na hofu ya msiba huo.
Alipopigiwa simu, ilipokelewa na mtu mwingine aliyesema kuwa mama huyo asingeweza kuzungumza kwa kuwa hali yake haikuwa nzuri.
Mama wa marehemu Janeth Kihoko, Devotha Mbutwa alisema juzi watoto wake walimpigia simu wakiomba ruhusa ya kwenda kwenye sherehe hiyo, kwamba na baadaye wangekwenda ufukweni.
“Niliwakatalia, wakapiga tena na tena, niliwaruhusu baada ya kuniambia kwamba wangekwenda hotelini tu bila kupita ufukweni. Kilichonishangaza baadaye nilipigiwa simu na kupewa taarifa za kifo cha binti yangu,” alisema kwa majonzi.
Mama huyo alisema hakukuwa na taarifa zozote alizopewa na jirani yake kuhusu sherehe hiyo.Msemaji wa familia hiyo, John Mbugi alisema mwili wa Janeth Kihoko unatarajiwa kuzikwa kesho katika Kijiji cha Viwengi, Wilaya ya Kilolo, Iringa.
Msemaji wa familia ya Ndimbumi Sisala, Lugano Mwakyosi alisema mwili wa binti yao utasafirishwa leo mchana kwenda Mbeya kwa mazishi yatakayofanyika kesho.
Kwa upande wa familia ya Eva Mwakatobe, baba wa marehemu, Nicholaus Mwakatobe alisema: “Mpaka saa hii sijaona polisi wakinihoji wala kufika kumhoji yule mama, bado yupo hapa mtaani na aliwachukua watoto bila idhini ya wazazi,” alisema Mwakatobe.
Meneja wa Hoteli ya Landmark, Moshi Mbully alisema vifo vya watoto hao ni ajali iliyotokea ghafla kwani mabwawa ya kuogelea huwa na walinzi wawili mpaka watatu.
“Tunasikitika sana kutokana na ajali hii, tunafuatilia kwa ukaribu msiba huu na tayari tumeshakutana na familia zote tatu. Mbaya zaidi watoto walikatazwa zaidi ya mara tatu wasielekee eneo lenye maji mengi lakini kwa bahati mbaya walikaidi,” alisema Mbully.
EmoticonEmoticon