REAL MADRID YAWALETA DAR FIGO NA SALGADO KUJA KUKIPIGA MECHI YA KIRAFIKI



Mmoja wa wachezaji nyota duniani, Luis Figo.

WATANZANIA watapata nafasi ya kumshuhudia mmoja wa wachezaji nyota duniani, Luis Figo akikipiga kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kabla ya mwaka huu kuisha.
Figo anatarajia kutua nchini mwishoni mwa mwaka huu kama makubaliano yatafikiwa kati ya Real Madrid na waandaaji wa ziara ya timu ya wakongwe ya Real Madrid kuja kucheza mechi ya kirafiki hapa nchini.
Beki nyota Michell Salgado.
Figo atakuwa katika kikosi cha Real Madrid pamoja beki nyota Michell Salgado na nyota wengine kama Christian Karembeu, raia wa Ufaransa.
Mmoja wa maofisa wa Real Madrid ambaye hushughulikia ziara za timu ya wakongwe, Rayco Garcia ambaye alitua nchini siku tatu zilizopita kufanya ukaguzi, amelithibitishia gazeti hili kuhusiana na ziara hiyo.
“Nimekuja kufanya ukaguzi, timu ya wakongwe ya Real Madrid haijawahi kufanya ziara Afrika. Lakini hata sasa ratiba ni sehemu mbalimbali kama Ulaya na Marekani. Kama ikija hapa, basi itakuwa mara ya kwanza barani hapa.
“Timu iko tayari kuja kulingana na ratiba, ila tunasubiri ambao wataandaa ziara hiyo. Shirikisho la soka la hapa (Tanzania), linajua kuhusiana na suala hilo na tumeelezwa tunashughulikia,” alisema Garcia aliyewahi kukipiga timu ya vijana ya Barcelona na Real Madrid.
Kuhusiana na wachezaji nyota, Garcia alisema Figo, Salgado, pia Fernando Hierro na wengine wengi watakuja lakini Zinedine Zidane anayefundisha Real Madrid na Roberto Carlos, kocha wa Besiktas ya Uturuki wametoa udhuru.
“Zidane na Carlos hawatakuja labda itokee mabadiliko ya ratiba au wakati timu inakuja wakiwa na nafasi. Lakini nyota wengine wote wako tayari kuja na timu imekuwa ikifanya mazoezi mara mbili kwa wiki pale Santiago Bernabeu,” alisema Garcia.
Garcia aliondoka nchini jana mchana na kusema ameridhika na mazingira na atakachosubiri ni kuthibitishiwa kutoka TFF na kwa waandaaji kama timu hiyo ije au la.
Previous
Next Post »