Na: Markus Mpangala
IMEZOELEKA kuwa katika jamii yetu mafanikio
yanaweza kupatikana kwa njia ya kutafuta ajira mara baada ya kutimu masomo.
Lakini kwa Meshack Maganga ambaye ni mkazi wa Iringa hali imekuwa tofauti na
amedhihirisha kuwa msomi yeyote anaweza kuleta mabadiliko ndani ya jamii bila
kutafuta ajira serikalini ama popote. Pia anadhihirisha kuwa maisha
yanapatikana mahali popote si lazima kuishi maeneo ya mjini.
Fuatilia
mahojiano haya;- MTANZANIA: Mkoa wa Iringa unasifika kwa kilimo cha miti ambazo
hutumika kwa nguzo za umeme, mbao, hewa ya ukaa na kadhalika.
Meshack Maganga, wewe ni miongoni mwa
wanaojihusisha na kilimo cha miti, ulianza lini shughuli hii na nini
kilikuvutia?
MAGANGA:
Kabla sijaanza kilimo cha miti, nilianza na kilimo cha mboga mboga mwaka 2011,
(baada ya kuhitimu masomo ya chuo kikuu hapa, Iringa), katika kijiji cha
Kalenga, pia nilianza kufuga kuku Iringa mjini, baada ya hapo kaka yangu
alianza kunihimiza na kunihamasisha kuhusu kilimo cha miti, wakati huo yeye
alikuwa akijihusisha na kilimo hicho. Nilibahatika pia kukutana na Rais wa
wapanda miti mkoani Iringa Mzee Chang’a (Rich Dad) ambaye alinifundisha kilimo
cha miti na kunipatia hamasa kubwa sana na pia alinisaidia kupata miche. Na
baadaye nikaanza ushirikiano na rafiki yangu Albert Sanga ambaye
anajishughulisha sana na kilimo cha miti. Baada ya kupata pesa mwaka huo,
nilinunua shamba la ekari 10 na kuzipanda miti ya mbao kutokana na pesa
niliyopata baada ya kuuza matango niliyolima kijijini Kalenga. Nikaongeza bidii
zaidi ya kulima matango na kununua mashamba mengi zaidi, mpaka mwaka huu 2013,
tayari nilikuwa nimenunua ekari za kutosha zenye miti ndani. Lengo langu ni kubwa
sana, nimepania kuwa na ekari nyingi zaidi zenye miti itakapofika 2018. Pamoja
na kuungana na serikali na dunia kwa ujumla katika kulinda mazingira,
ninakithamini kilimo cha miti katika eneo hili ili kujiandaa kiuchumi kwa faida
yangu na jamii inayo nizunguka. Nina malengo ya kugugusa jamii. Kwa hiyo huu ni
mwaka wa tatu tangu nilipo jiajiri kwenye kilimo cha miti.
MTANZANIA: Unaweza kuwaeleza wasomaji wetu na
watanzania kwa ujumla juu ya faida ya kilimo cha Miti?
MAGANGA: Kilimo cha miti, kina faida sana,
pengine baadhi ya watanzania wa ndani na nje ya nchi wengi wao hawajabahatika
kusikia faida ya kilimo hiki, ama wengi wao wamekisikia na kuzifahamu faida za
kilimo cha miti. Wanashindwa waanzie wapi, na ndio maana mpaka sasa wanaolima
miti ni watanzania wachache sana, na wale waliojitokeza kulima miti ndio
mamilionea wa miaka michache ijayo. Mwaka jana nilitoa somo la “Usikubali kuwa
mnyonge wa kiuchumi ndani ya Tanzania” kama njia ya kuhamasisha kilimo cha
miti. Nilisema kuwa Kilimo cha miti ya mbao, nguzo, milunda na miti ya kuni na
dawa, kimepata umaarufu wa ghafla miaka ya hivi karibuni kutokana na sababu
mbalimbali ikiwemo ongezeko la mahitaji ya mazao ya miti na changamoto ya
mazingira. Hapa nchini mkoa wa Iringa ni moja ya mikoa maarufu inayoongoza kwa
misitu mikubwa ya kupandwa. Miti inatumika kwa mbao, nguzo za umeme, nguzo za
kujengea pamoja na utengenezeaji wa karatasi na madawa. Hivi sasa kumeibuka
fursa nyingine mpya ambapo mashirika ya kimazingira kutoka Magharibi yananunua
hewa ya ukaa. Kwa maana hiyo unaweza kupanda shamba la miti halafu ukawa
unakusanya dola kwa kuuza hewa ukaa wakati ukisubiri miti ikomae uvune mbao,
nguzo ama miti ghafi ya kutengenezea karatasi. Hii ni sawa na kutengeneza pesa
ukiwa umelala nyumbani kwako (Making money while sleeping). Mbali na kuuza hewa
ukaa, vile vile unaweza kufuga nyuki na kuendelea kuvuna asali.
MTANZANIA:
Kuna changamoto gani katika kilimo cha miti na uchumi kwa ujumla?
MAGANGA:
Nimekutana na changamoto nyingi sana baadhi ya changamoto nilizo kutana na nazo
tangu nilipoanza kilimo cha miti; kukosa pesa za kutosha hasa kipindi cha
kupanda miche mipya kinapoaanza, maana unapopanda miti mpya unatakiwa uwe na
pesa ya kutosha. Changamoto nyingine ni tatizo la usafiri, mashamba mengi ya
miti yapo nje ya mji wa Iringa, unatakiwa usafiri kilomita nyingi kwa siku
mpaka kufika sehemu yalipo mashamba hasa katika wilaya ya Mufindi na Kilolo,
wakati wa masika kama haya barabara haipitiki kwa sehemu kubwa. Pia kuna
changamoto ya moto wa msituni, kipindi cha nyuma kabla ya ujio wa makampuni
makubwa yanayojihusisha na kilimo cha miti, kulikuwa na tatizo kubwa la moto
kuchoma baadhi ya mashamba, lakini kwa sasa wananchi wameelimika sana, hakuna
tena tatizo la moto kama zamani, moto ukitokea ni ule moto wa bahati mbaya.
Lakini changamoto hii kwangu ilikuwa fursa, sikurudi nyuma mpaka leo naona
mafanikio.
MTANZANIA:
Umeeleza awali kuwa ni watanzania wachache sana wanajihusisha na kilimo cha
miti. Lakini una ushauri gani kwa kwao na watanufaikaje kiuchumi kupitia kilimo
cha miti?
MAGANGA:
Vijana wanaoishi mkoani Iringa na Tanzania kwa ujumla na pia vijana watanzania
waliokimbilia nje ya nchi, wana nafasi kubwa sana ya kunufaika na uwekezaji
kwenye kilimo cha miti, na hapa ninaongelea vijana wa kike na wa kiume, waliomo
kwenye ajira rasmi na wale waliojiajiri kama mimi, na wale waliopo masomoni
wasibweteke na mikopo wanayoipata huko wanakosoma. Watanzania wanaweza
kunufaika na kilimo cha miti kwa aina mbalimbali, lakini ninaweza kuzitaja
chache hapa. Unaweza kuamua kuuza miti (magogo) ambapo kwa nguzo kwa mti mmoja
uliokomaa vizuri unauzwa kuanzia 80,000/-. Kwa upande wa miti ya mbao na
karatasi, iliyokomaa vizuri mti mmoja huuzwa kuanzia 60,00 kutegemeana na
umbali wa shamba. Shamba linapokuwa mahali kusikofikika bei ni ndogo zaidi).
Namna ya pili ya uvunaji ni kuvuna mwenyewe kwa maana ya ama kupasua mbao au
kutengeneza nguzo za umeme za kuuza. Mvunaji inakulazimu uwe katika biashara
kamili ya mbao kwa sababu utahitaji mashine, leseni, vibali na taratibu
nyingine,na hapa ndio penye faida kubwa sana. Soko la mbao na nguzo/mirunda
liko juu sana na uhitaji wake ni mkubwa kuliko uzalishaji. Nadhani unatambua
kuwa mahitaji ya bidhaa za miti yameongezeka kwa kasi sana miaka ya hivi
karibuni. Hata hivyo kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika na wataalamu wakiwemo
SUA wanatueleza kuwa soko la bidhaa za misitu (mbao, nguzo n.k) litaendelea
kupanda bila kushuka kwa miaka 25 ijayo kuanzia mwaka 2010. Kama wawekezaji
tunakuwa kuwa na hamasa chanya katika hilo ijapokuwa hatuachi kuweka tahadhari
ya ‘risks’ (hasa market changes) kama ambavyo ni kawaida kwa biashara yeyote
duniani.
MTANZANIA:
Umeeleza kuna mashirika yananunua hewa ya ukaa. Pia umesema soko la mbao ni
kubwa na lina manufaa kwa anayehitaji. Je unadhani kitu gani kinaweza kusaidia
kubadilisha fikra za watanzania kuelewa faida itokanayo na kilimo cha Miti?
MAGANGA:
Kwa sasa dunia imebadilika sana na itaendelea kubadilika, iwapo sisi
tutajifanya hatuyaoni mabadiliko hayo na kuendelea na mitazamo ile ile ya zama
za kati za mawe, ikumbukwe kwamba, janga kubwa duniani si kifo wala ajali, bali
ni kuishi bila malengo. Vijana wadogo wake kwa waume wanaohitimu vyuo
mbalimbali wapo bize kusaka ajira, na wale ambao bado wapo shuleni na vyuoni na
wao wana ndoto za kupata ajira (idadi yao ni kubwa sana).
Na
baadhi ya waliopo kwenye ajira wamechoshwa na ajira zao,wanafokewa kama watoto,
wanakosa muda wa kufanya mambo yao, na wengine wanalalamikia mishara midogo.
Serkali imetoa fursa kwa wananchi kumiliki ardhi na msisitizo upo kwenye kilimo
lakini bado wengi wao wanaona kilimo ni kama kazi ya watu wasio soma na
waliokosa cha kufanya, wanaona bora watembeze bahasha kuomba kazi ambazo kwa
hakika ni chache sana kuliko kujiajiri.
Mbaya
zaidi waliopo kwenye ajira wake kwa waume, wazee wenye umri wa miaka 60 na
kuendelea hawapo tayari kuachia ajira zao. Unajua ni kwanini hawataka kuachia
ajira zao? Bado wanajiandaa, na wengine hawajapata mitaji miaka nenda rudi.
Kwanini usiwekeze kwenye kilimo cha miti? Pale mkoani Morogoro kuna fursa ya
kilimo cha Mitiki, Tanga kuna fursa ya kilimo cha miti ya mbao, Ruvuma na
kwingineko, ama tunasubiri ardhi iishe ndio tuanze maneno? Rafiki yangu, Albert
Sanga, aliwahi kusema Mazoea na utamaduni wa watanzania wengi kudhani kwamba
tunaonewa. Mtindo wa kuishi maisha ya kutaka kuhurumiwa yanatupotezea muda
wenye thamani.
Tumekuwa tukilalamika kuwa wageni (wanaokuja
kwa jina la wawekezaji) wanatupora ardhi; lakini tusichokitafakari ni hiki,
“Mimi kama mtanzania kwa nafsi yangu na kwa uwezo wangu nimefanya nini cha maana
katika ardhi ninayoweza kuipata hapa nchini ama ninayomiliki?”.
Kumbuka
kuwa dunia haina huruma kwa mwanadamu anaye lala tu huku akilaumu serkali, ama
akiendelea kukesha akifanya maombi, bila kufanya maana Mungu hana huruma na
watu wavivu ama akiendelea kuwalaumu wazazi wake ama kozi aliisoma chuo kikuu,
ama akimsingizia shetani kila kukicha. Mtanzania yeyote wa kada yoyote
atakayependa kuungana na sisi katika kilimo cha miti ili kutunza mazingira
wakati tunasubiri kuvuna miti, tunamkaribisha Iringa aje kujifunza kwenye
mashamba yetu kisha atafanya maamuzi.
Nimekuwa nikirudia kauli ya Baba yangu
(Mwenyekiti wa wapanda miti-Iringa) maarufu kama ( Rich Dad) ambaye siku za
karibuni amepewa Tuzo ya Rais kwa kuwa mpandaji namba moja wa miti na utunzaji
wa mazingira. Kila mwanzo wa msimu wa kupanda miti amekuwa akitoa msaada kwa
watanzania wa ndani na nje ya Tanzania kuwasadia kupata eneo la kupanda miti na
miche. Watu wasikubali kuwa wanyonge wa kiuchumi ndani ya Tanzania.
EmoticonEmoticon