Chama Cha Mapinduzi kimezindua kampeni katika Jimbo la Chalinze kwa kishindo, huku viongozi wa kitaifa wakimwombea kura, Ridhiwani Kikwete ili awaletee maendeleo
Katika mkutano huo, Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete aliwataka Wanachalinze kutomuumiza tumbo kwa kumnyima ridhaa mwanaye Ridhiwani ambaye anaamini atatatua kero mbalimbali zinazowakabili wakazi wa jimbo hilo.
Mama Salma alitoa ombi hilo katika viwanja vya Polisi Chalinze, kuwa yeye kama mama mzazi ana kila sababu ya kumwombea kijana huyo kura zote za ndiyo kutokana na kuwa na uwezo wa ushawishi wa masuala mbalimbali na pia ni mpenda watu popote alikokuwa akipita.
Alisema amefika katika viwanja hivyo kwa sababu kuu tatu, moja ni mama mzazi wa mgombea, pili ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kupitia Mkoa wa Lindi na tatu ni kwa vile yeye ni mke wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.
“Ndugu zangu Wanachalinze, leo tumbo linaniuma sababu ya mwanangu, lakini namjua mtoto wangu ni mpenda watu, popote alikopita alieneza upendo na pia ana uwezo mkubwa wa kuongoza na kujenga ushawishi wa masuala mbalimbali ya maendeleo,” alisema na kuongeza:
“Nawaomba sana msiniangushe mzazi mwenzenu, kihemba na mwanaye na pia uchungu wa mwana ajue mzazi namwombea kura zote Ridhiwani,” alisema Mama Salma.
CHANZO:MWANANCHI
EmoticonEmoticon