Klabu ya Manchester United huenda ikafanikiwa kumpata kirahisi kiungo kutoka nchini Ujerumani na klabu ya Bayern Munich Toni Kroos ambae hii leo ameweka wazi nia yake ya kutaka kucheza soka kwenye ligi ya nchini Uingereza msimu ujao.
Man utd wanatajwa katika harakati za kumnasa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24, kufuatia meneja wa klabu hiyo ya Old Trafford, David Moyes, kuwa na mipango mizuri ya kutaka kumsajili tangu mwanzoni mwa msimu huu lakini alikutana na ugumu kutoka kwa viongozi wa The Bavarians.
Toni Kroos amethibitisha kuwa tayari kuelekea nchini Uingereza, huku ikifahamika yupo kwenye mazungumzo na viongozi wa klabu ya Bayern Munich ya kusaini mkataba mpya, lakini kauli yake umeanza kuhisiwa huenda mustakabali wa kuendelea kubaki Allanze Arena ukawa haupo tena.
Hata hivyo kiungo huyo amesema mpaka sasa hakuna mazungumzo yoyote ambayo yameshafanikisha azma yake ya kuendelea kubaki nchini Ujerumani akiwa na Bayern Munich, hali ambayo inampa namna ya kuanza maisha mapya katika ligi ya nchini Uingereza.
Lakini pamoja na klabu ya Man Utd kupewa nafasi kubwa ya kumsajili Toni Kroos, bado kuna mtihani mgumu unaowakabili kufuatia kiungo huyo kuweka bayana suala la kuhitaji kucheza kwenye klabu ambayo itashiriki michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu ujao.
Kama itakumbukwa vyema Toni Kroos ndie aliefunga bao la kwanza wakati wa mchezo wa mkondo wa kwanza wa ligi ya mabingwa barani Ulaya hatua ya 16 bora, dhidi ya Arsenal majuma mawili yaliyopita huko kaskazini mwa jijini London.
EmoticonEmoticon