Dave Whelan awapiga mkwara Arsenal, ni baada ya kuitotesha Man City


Mmiliki wa klabu ya Wigan Athletics Dave Whelan amewatumia salamu Arsenal kwa kuwaambia wasitarajie mteremko katika mchezo wa hatua ya nusu fainali ya kombe la FA, baada ya kikosi cha klabu yake kufanikiwa kuifunga Man City kwenye mchezo wa hatua ya robo fainali hapo jana.
Dave Whelan ametuma salamu hizo kwa kusema anatambau kikosi cha Wigan kinapewa nafasi finyu ya kutinga katika hatua ya fainali ya michuano hiyo lakini kwake haamini kama mawazo hayo ni sahihi.
Whelan amesema hawana budi kuwaheshimu Arsenal ambao watakuna nao kwenye hatua ya nusu fainali mwezi ujao, kutokana na ukubwa wa jina lao lakini katu hawatohofia lolote kwa kisingizio cha yanayo zungumzwa na vyombo vya habari pamoja na wadau wa soka nchini Uingereza.
Hata hivyo kiongozi huyo amesema kama kikosi chake kimefanikisha azma ya kuiondosha Man city kwenye michuano ya FA, anaamini hakuna litakalo shindikana mbele ya Arsenal katika uwanja wa Wembely.
 “Msimu uliopita tulipokutana na Man city, kila mmoja alitudharau na kuamini tulikuwa hatuna namna ya kuwafunga, lakini tulifanikiwa, na msimu huu tumekutana nao bado tumeshinda tena, sasa iweje Arsenal wanaanza kupewa nafasi ya kutufunga kabla hatujacheza?”Alihoji kiongozi huyo.
Katika hatua nyingine Dave Whelan amekipongea kikosi cha klabu yake kwa kusema kilionyesha soka safi katika mchezo wa jana mbele ya Man City ambao walikua nyumbani huko Etihad Stadium.
Whelan amesema anaamini kilichofanyika katika uwanja wa Etihad hapo ni kazi nzuri ambayo imefanywa na meneja kutoka nchini Ujerumani Uwe Rösler ambae alimkabidhi kikosi mara baada ya kuondoka kwa Roberto Martinez mwanzoni mwa msimu huu.
Amesema lengo lao msimu huu ni kutaka kurejea kwenye ligi kuu ya soka nchini Uingereza lakini kikubwa wanachokihitaji kwa sasa ni kuhakikisha wanatetea ubingwa wa kombe la FA, kutokana na kuwa na meneja mwenye sifa za kukamilisha maazimio hayo mawili.
Mbali na mafanikio yaliyofikiwa ya kutinga katika hatua ya nusu fainali, klabu ya Wigan kwenye msimamo wa ligi daraja la kwanza nchini Uingereza ipo kwenye nafasi ya saba kwa kuwa na point 52, ikiwa ni tofauti ya point 22 dhidi ya Leicester city walio kileleni.
Previous
Next Post »