PIGO NDUGU 12 WAFA KATIKA AJALI YA GARI WAKATI WAKIELEKEA MSIBANI



Mji wa Hedaru uliopo wilayani Same mkoani Kilimanjaro, jana ulizizima kwa vilio na simanzi baada ya waombolezaji 12 wote ndugu, kufariki dunia kwa ajali ya barabarani.
Waombolezaji hao wanawake, walipewa lifti ya gari na Diwani wa Kata ya Hedaru, Gerard Mgwena (CCM), kwa ajili ya kuwapeleka msibani eneo la Majengo ambako mtu mmoja alifariki kwa kusombwa na maji.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro (RPC), Robert Boaz alithibitisha ajali hiyo akisema ilitokea juzi saa 2:00 usiku na kwamba ilikuwa mbaya zaidi tangu kuanza kwa mwaka 2014.
“Ni ajali iliyohusisha magari matatu kwa wakati mmoja…; watu 11 walifariki pale pale na mwingine alifariki dunia leo (jana), asubuhi Hospitali ya Rufaa ya KCMC,”alisema Boaz.
Hata hivyo, alisema hakuwa na nafasi nzuri ya kufafanua kwa undani ajali hiyo kwa vile alikuwa nje ya Mkoa wa Kilimanjaro na kuelekeza atafutwe Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa (RTO), Joseph Mwakabonga.
Akizungumza kwa niaba ya RPC, Mwakabonga alisema, lori aina ya Mitsubish Fusso lililokuwa likitokea Moshi kwenda Dar liligonga kwa nyuma gari aina ya Toyota Hilux Pick-Up.
Alisema kuwa baada ya kuligonga gari hilo lililowabeba waombolezaji hao, nalo lilisukumwa na kwenda kuligonga lori aina ya Scania lililokuwa na tela lake.
Lori hilo aina ya Scania lilikuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Moshi likiendeshwa na dereva wake, Gabriel David. Madareva wawili wa Toyota Pick-Up na Toyota Fusso wote hawajulikani waliko.
Taarifa zilizopatikana baadaye, zilisema dereva wa Fusso alikuwa amelazwa katika Hospitali ya KCMC, wakati Kigogo wa CCM aliyekuwa amewabeba waombolezaji akilazwa hospitali moja jijini Arusha.
Mwakabonga aliwataja waliofariki kuwa ni Stella John(45), Salma Kizoka (33), Marry Senzige (49), Neema Daniel (52), Rehema George (29) na Sophia Mbike (51).
Wengine ni Ritha Kalani (55), Mama Kalani Stephano (55), Kolina Mmatha(55), Bahati Daud(25) na Farida Kiondo mwenye umri wa miaka 25.
Majeruhi mmoja, Maria John (33) ambaye ni miongoni mwa watu 10 waliojeruhiwa, alifariki dunia jana asubuhi katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC alikolazwa kwa ajili ya kuokoa maisha yake.
Previous
Next Post »