MAHAKAMA Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imefuta kwa mara ya pili maombi ya kufanya marejeo kuhusu kuliondoa shitaka la kukaidi amri halali iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, dhidi ya Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda (pichanibaada ya kufunguliwa kwa kukiuka sheria.
Kadhalika maombi hayo yamefutwa baada ya kukiuka kifungu cha 372 kidogo cha (2) cha Mwenendo wa Sheria za Makosa ya Jinai (CPA) ambacho hakiruhusu maombi hayo kupelekwa Mahakama Kuu.
Akitoa uamuzi wa mahakama, Jaji Augustino Mwarija alisema maombi hayo yamefunguliwa kwa kukiuka kifungu cha 372 kidogo cha (2) na kwamba amekubali pingamizi la Jamhuri na kuyafuta. Upande wa Jamhuri unaongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Bernad Kongola.
“Naona maombi haya yameletwa kwa kukiuka kifungu cha 372 kidogo cha (2) cha CPA, nakubaliana na pingamizi la Jamhuri … hatimaye mahakama imeona maombi yameletwa bila kuzingatia sheria nayafuta” Alisema wakati akisoma uamuzi uliyofuta maombi ya mshtakiwa huyo.
Akifafanua zaidi alisema kifungu hicho siyo sahihi kwamba kinazuia uletaji wa maombi mahakamani dhidi ya amri ya awali na ya muda zinazofanya mahakama za chini isipokuwa amri ambazo zinahitimisha shauri lote la jinai.
“Kwa sababu hiyo hoja ya mleta maombi kwamba amri imetolewa kuhusu pingamizi la awali siyo sahihi na siyo tafsili ya kifungu hicho uamuzi huo haumalizi kesi… Sheikh Ponda ana mashtaka matano ya jinai na uamuzi wa Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate haukusu pingamizi la awali haukumaliza mashtaka “alisema Jaji Mwarija.
Mapema Desemba 11, mwaka 2013, kwa mara ya kwanza mahakama hiyo iliyoketi chini ya Jaji Rose Teemba iliyafuta maombi hayo baada ya upande wa Jamhuri kutoa pingamizi la awali kwamba kiapo kilichoambatana na maombi hayo kilikuwa na mapungufu ya kisheria ikiwemo kutokuwa na tarehe pamoja na jina la mtoa kiapo.
Jaji Teemba alisema mara alipopokea jalada la kesi hiyo aliona mapungufu hayo lakini siku Desemba 2, mwaka huu alishangaa kuona kiapo kimefanyiwa marekebisho.
Hata hivyo, Desemba 13, mwaka 2013, Sheikh Ponda kupitia mawakili wake Obadia Hamidu na Juma Nassoro alifungua maombi mengine ambayo jana yamefutwa baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) kuwasilisha pingamizi la awali la kupinga maombi hayo.
DPP aliwasilisha pingamizi la awali dhidi ya Sheikh Ponda akidai maombi yake hayana mashiko ya kisheria na aliomba mahakama kuyafuta.
Katika pingamzi hilo, DPP aliomba kuwa maombi ya Sheikh Ponda hayaruhusiwi kusikilizwa mahakamani hapo chini ya kifungu cha 372 kidogo cha (2) cha Mwenendo wa Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA), kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Kifungu hicho kinaeleza kwamba mtu hataruhusiwa kuwasilisha maombi yoyote ya marejeo ambayo yanatokana na maamuzi au amri ya mahakama ya chini ambayo hayakumaliza kesi.
Akijibu hoja za DPP, wakili wa utetezi Juma alidai kuwa maombi hayo yana mashiko ya kisheria na kwamba mshtakiwa ana haki ya kusikilizwa na mahakama hiyo.
Katika kesi ya msingi, Sheikh Ponda anakabiliwa na mashtaka ya kukaidi amri halali, kuharibu imani za dini, kushawishi na kutenda kosa. Kesi hiyo inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.
Awali, Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP), aliwasilisha ombi la kuzuia dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo kwa sababu ya maslahi ya nchi na usalama wake mwenyewe.
Baada ya Shekh Ponda kunyimwa dhamana wakili wake, Nassoro aliwasilisha ombi jingine mahakamani hapo la kufuta shitaka la kwanza ambalo ni kukaidi amri halali akidai kuwa mahakama hiyo haina uwezo kisheria kusikiliza vinginevyo lifunguliwe katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Akitoa sababu za kutaka kufutwa ama kuhamishia shtaka hilo katika Mahakama ya Kisutu, Wakili Nassoro, alidai kuwa amri hiyo halali anayodaiwa kuivunja mteja wake ilitokana na hukumu iliyotolewa katika Mahakama ya Kisutu Mei, mwaka 2013 ambayo Ponda alihukumiwa kifungo cha nje cha mwaka mmoja na kutotakiwa kufanya kosa lolote la jinai katika kipindi cha mwaka mmoja. Hata hivyo, Hakimu Kabate alitupilia mbali maombi hayo na Sheik Ponda ya kufanya marejeo Mahakama Kuu dhidi ya shitaka hilo.
EmoticonEmoticon