HII NDIYO TAARIFA KAMILI YA AJALI ILIYOHUSISHA MAGARI MATANO NA KUUA WATU 22 MKOANI PWANI.

Wananchi wakiangalia daladala iliyopata ajali juzi usiku katika eneo la Kijiji cha Mkupuka, wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani. Picha na Amini Yasini.
RUFIJI
SIKU moja baada ya ajali kuua watu 12 wilayani Same, ajali nyingine mbili mbaya zilizohusisha magari matano zimetokea katika eneo moja wilayani Rufiji na kuua watu 22, akiwamo kondakta wa gari aina ya Toyota Hiace ambaye kichwa chake kimetenganishwa na kiwiliwili.
Ajali hizo zilizopishana kwa dakika chache zilitokea juzi saa 1:00 jioni katika Kitongoji cha Mkupuka, Kata ya Kibiti na zilisababisha vifo vingi kutokana na watu 14 waliojeruhiwa katika ajali ya kwanza iliyoua watu saba, kukanyagwa na gari jingine wakati wakisubiri kupandishwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser la Idara ya Maliasili ili kupelekwa hospitali.
Habari kutoka Kituo cha Afya cha Ikwiriri zinaeleza kuwa miili ya watu wawili ilitenganishwa kichwa na kiwiliwili, maiti tano zilikuwa na vichwa vilivyopasuka na maiti nyingine zilikuwa zimekatikakatika mifupa.
“Hii ni ajali mbaya kati ya ajali ambazo nimewahi kuziona maishani,” alisema mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, Frank Sixmund Mlangira (30) ambaye amelazwa Hospitali ya Mchukwi na ambaye ni dereva wa gari aina ya Toyota Land Cruiser la Idara ya Maliasili ambalo liligongwa katika ajali ya pili wakati likichukua majeruhi kuwapeleka hospitalini. “Dereva wa Hiace alikatwa kichwa na kikatenganishwa na kiwiliwili.”
Ajali ilivyokuwa
Kwa mujibu wa mashuhuda, ajali ya kwanza ilitokea wakati gari ya abiria aina ya Toyota Hiace lilipojaribu kukwepa lori lililokuwa limeegeshwa pembeni mwa barabara na badala yake kugongana uso kwa uso na lori aina ya Mitsubishi Fuso lililokuwa likielekea Dar es Salaam.
Katika ajali hiyo ya kwanza watu saba walikufa papo hapo na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa.
Wakati juhudi zikifanyika kuokoa majeruhi na kutoa miili ya waliofariki, basi jingine lililokuwa kwenye mwendokasi likitokea Lindi kwenda Dar es Salaam, liliwakanyaga majeruhi 14 waliokuwa wakisubiri msaada na baadaye kugonga gari la Idara ya Maliasili lililokuwa likipakia majeruhi kuwapeleka hospitali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema dereva mmoja anashikiliwa na polisi wilayani hapa kwa mahojiano.
Kamanda Matei alisema kuwa maiti 19 zimehifadhiwa katika Kituo cha Afya cha Ikwiriri na wawili wapo Kituo cha Afya Kibiti.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mchukwi, Dk. Zakaria Lukeba alisema walipokea majeruhi 13 wa ajali hiyo na kuongeza kuwa kati ya majeruhi hao, wawili walithibitika kuwa walishafariki kabla ya kufika na kufanya idadi ya waliofariki kufikia 23, idadi ambayo inatofautiana na takwimu za Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ambazo zinaonyesha waliofariki eneo la tukio ni 21. Jana mchana majeruhi mmoja alifariki na idadi ya waliofariki kufikia 22.
Alisema majeruhi watano wamehamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi na kuongeza kuwa majeruhi sita tu ndio waliobaki hospitalini hapo wakiendelea na matibabu.
SOURCE MWANANCHI
Previous
Next Post »