Emmanuel Okwi asajiliwa na Yanga .




Klabu ya Dar es salaam Young Africans imekamilisha usajili wa mchezaji wa zamani wa Simba ambaye pia ni mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda Emanuel Arnold Okwi toka klabu ya Sports Club Villa ya Uganda .
Taratibu za kumsajili mchezaji huyo zimekamilika ambapo amesaini mkataba wa miaka miwili utakamomfanya aichezee Yanga mpaka mwishoni mwa mwaka 2015 .
Usajili huu unafunga idadi ya wachezaji wa kigeni wa Yanga ambapo anaungana na Didier Kavumbangu, Haruna Niyonzima , Mbuyi Twite na Hamis Kiiza.

Zaidi ya hapo unakuwa usajili wa mwisho wa Yanga katika dirisha dogo la usajili wakati huu ambao ligi imesimama baada ya mapumziko ya kipindi cha sikuu baada ya kumalizika kwa raundi ya kwanza . Dirisha hilo linafungwa usiku wa kuamkia tarehe 16 /12/2013 .
Okwi atachelewa kuungana na wachezaji wenzie wa Yanga baada ya kulazimika kubaki nchini Uganda ambako anamalizia upigaji picha za matangazo anayoyafanya kwa niaba ya kampuni moja ya simu nchini humo ambayo Okwi ana mkataba nayo.
Okwi aliondoka Simba baada ya kuuzwa kwenda klabu ya Etoile Du Sahel ya Tunisia ambayo hakukaa nayo muda mrefu baada ya kuvunja mkataba kabla ya kuidhinishwa na FIFA kujiunga na Sports Club ambayo leo hii imemuuza Okwi kwa ada ya uhamisho ya Dola Za Kimarekani 20,000.

Usajili huu unamfanya Okwi kuikosa michuano ya kombe la mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani ambapo Uganda itashiriki mashindano hayo huko Afrika kusini mwakani.
Previous
Next Post »