“Mawasiliano ni
kitu/nyenzo muhimu katika uhai wa chombo chochote kile” Katika karne ya 21 ya maendeleo ya sayansi na teknolojia suala la
mawasiliano limeshika kasi kubwa kwa kila Mwananchi na Hata wadau wake. Kwa
namna hii, mawasiliano limekuwa ni jambo muhimu sana ambalo huwezesha mtu na
mtu kupashana habari, wizara kutoa taarifa mbalimbali kwa wananchi kuhusu
matukio, na hata malengo na mikakati iliyojiwekea.
Kwa hapa kwetu nchini, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(Tanzania Communication Regulatory
Authority – TCRA ) ndicho chombo kinachosimamia biashara ya mawasiliano kwa
njia ya simu, matangazo ya redio na televisheni, utoaji wa huduma za posta,
ugawaji na usimamizi wa masafa ya matangazo ya redio pamoja na teknolojia ya
habari na mawasiliano. Chombo hiki kina majukumu ya kulinda na kusimamia
maslahi ya watumiaji wake na kusambaza taarifa mbalimbali za kiushauri na
kiulinzi kwa watumiaji wa mawasiliano na kwa Wizara mbalimbali za serikali.
Katika kufanikisha
shughuli mbalimbali za kiutendaji, Jeshi la Polisi nchi limejitahidi katika
kuhakikisha suala la mawasiliano na upashanaji habari kwa umma linazingatiwa.
Hii ni kwa nia ya kutoa fursa kwa wananchi kutumia nyenzo hii ya mawasiliano
kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusiana na matukio ya uhalifu,wahalifu,majanga,
ajali, na hata kutoa taarifa pindi waonapo kuna jambo au kitu wanachokitilia
mashaka. Je,ni mara ngapi mimi na wewe tunatumia nyenzo hii ya mawasiliano
katika kudhibiti na kuzuia vitendo vya uhalifu?au ni mara ngapi mimi na wewe
tunasaidia kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili kufanikisha utendaji wake?
Miaka ya hivi
karibuni Jeshi la Polisi Tanzania limezidi kuimarisha shughuli zake za
kiutendaji na kutoa fursa kwa wananchi kushirikiana na Jeshi hili ili kudhibiti
na kuzuia vitendo vya uhalifu kwa njia/dhana ya Polisi Jamii na Polisi Rafiki
pale wananchi wanapo shiriki kikamilifu katika ulinzi wa mali zao na maisha yao
kwa kushirikiana zaidi na Jeshi la Polisi. Dhana hii pia imetoa fursa kwa
wananchi kuwa huru kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kwa Jeshi la Polisi
zinazo husiana na uhalifa, wahalifu au, matukio mbalimbali kama vile ajali za
barabarani, majanga na nyingine za
kiusalama.
Katika kuhakikisha
Wananchi wana shiriki katika utoaji wa taarifa, Jeshi la Polisi kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali ndipo lilipoanzisha Miradi mbalimbali ambayo
inafanya kazi sambamba na kwa ukaribu
zaidi na wananchi ili kuweza kusaidia katika mawasiliano na utoaji wa taarifa. Baadhi
ya miradi hiyo ni pamoja na; Usalama wetu kwanza, mradi wa safiri salama, mradi
wa ukamataji salama,klabu marafiki shuleni (Polisi Rafiki), huduma bora kwa
mteja (customer care), utii wa sheria bila shuruti, kuzuia ukatili wa kijinsia
(TPF-Net), kuzuia na kupambana na wahamiaji haramu, mazingira salama na mingine
mingi.
Kupitia miradi hii
ya Polisi Jamii, Jeshi limeweka wasimamizi na watendaji kwa kushirikiana na
wananchi na pia kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kufanikisha utendaji
wake. Uwepo wa miradi hii ni fursa pekee kwa wananchi kuwasiliana na kutoa
taarifa kwa Jeshi la Polisi ili kudhibiti uhalifu. Kwa kutekeleza hili Jeshi la
Polisi limeamua kutoa namba za simu za Makamanda wa Mikoa , wakuu wa polisi wa
wilaya na Wakuu wa Vikosi kama vile Kikosi cha Usalama Barabarani ili Wananchi
wawe huru muda na wakati wowote hata kama wapo safarini kutoa taarifa za
kiusalama ili kudhibiti matukio ya uhalifu na ajali zinazoweza kuepukika.
Matumizi ya nyenzo
hii ya mawasiliano imekuwa na nguvu sana katika kuleta mabadiliko ya kiutendaji
katika Jeshi la Polisi na kuongeza ufanisi. Kwani Jeshi limekuwa likipokea
taarifa, maoni, na changamoto mbalimbali kutoka kwa wananchi na wadau. Njia
hizi za mawasiliano zimeonekana kuwa zikitumiwa vizuri zitafanikisha malengo
yetu ya kudhibiti,kuzuia, na kupambana na uhalifu. Matumizi sahihi ya
usambazaji taarifa kwa kutumia simu za mkononi na mitandao ya kijamii, kwa sasa
ni sehemu pekee inayotoa fursa kwa wananchi kutoa taarifa, maoni na hata
changamoto ambazo Jeshi huzibadilisha kuwa ni fursa katika kuongeza ufanisi wa
kiutendaji.
Jeshi la Polisi
linazidi kutoa elimu kwa wananchi kutambua umuhimu wa Jeshi hili, kazi na
majukumu yake. Kwa njia ya mikutano ya Polisi Jamii na Polisi Rafiki, elimu
imeweza kutolewa na kuwafikia wananchi wengi katika maeneo mbalimbali. Pia
elimu ya utoaji salama wa taarifa imeendelea kutolewa katika Shule za Msingi na
Sekondari ili wanafunzi wajue wajibu wao na umuhimu wao katika Jeshi kwa njia
ya kutoa taarifa sahihi kwa lengo la kudhibiti uhalifu na vitendo vya uvamizi
katika Shule.
Wizara imeona
umuhimu wa chombo hiki na kuongeza wigo wa mawasiliano baina yake na wananchi.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Saidi Mwema akifungua mkutano wa siku mbili
wa Wakurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) wa shirikisho la Polisi
Kusini mwa Afrika (SARPCCO) alisema, “Watanzania wote wakitoa taarifa na
kuzipeleka katika mamlaka husika, kwa mujibu wa sheria za mwenendo wa jinai
kifungu namba 7, hatimaye watuhumiwa wataweza kushughulikiwa kwa mujibu wa
sheria”.
Ni wazi kuwa kila
mmoja wetu akishiriki katika utoaji wa habari, basi tunauwezo mkubwa wa
kuimarisha usalama katika maeneo mbalimbali na kudhibiti vitendo vya uhalifu. Pia
tutakuwa na uwezo mkubwa wa kulinda maisha yetu, mali zetu pamoja na kuokoa
mali zilizo katika mazingira ya kuibwa au kuporwa. Bila kushirikiana na
wananchi Jeshi bado litakuwa na kazi kubwa kwani wahalifu wamo ndani ya jamii
na wanaishi miongoni mwetu. Sote tuone tunayo sababu ya kushiriki katika ulinzi
kwa njia ya utoaji taarifa kwa mamlaka husika tukiamini kuwa “mawasiliano ni
nyenzo yenye nguvu” [communication is power].
Imetolewa
na:
[DIWANI ATHUMANI – ACP]
KAMANDA
WA POLISI MKOA WA MBEYA.
EmoticonEmoticon