MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesisitiza kuwa msimamo wake wa tozo ya Sh 1,000 kwa laini moja ya simu upo palepale na kuwataka wamiliki wa kampuni za simu kuhakikisha wanaendelea kutoza kodi hiyo japokuwa kesi ya kupinga agizo hilo ipo mahakamani. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Mlipa Kodi, Richard Kayombo alisema kodi hiyo itaendelea kutozwa kwa kuwa wanatimiza sheria iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Sitaki kufafanua zaidi kuhusiana na tozo hiyo, kwakuwa kwa sasa lipo mahakamani kisheria zaidi lakini cha msingi ni kwamba tumeagiza makampuni yote kuanza utekelezaji wa agizo hilo kuanzia Julai mwaka huu hadi hapo mahakama itakapotoa maamuzi mengine,” alisema Kayombo.
Wakati huo huo, Naibu Kamishna wa Kodi za Ndani, Generose Bateyunga alisema mamlaka hiyo itatoa adhabu kali kwa wafanyabiashara ambao watakaidi kutumia mashine za kieletroniki ambapo muda wa mwisho wa kununua na kutumia mashine hizo ni Novemba 15, mwaka huu.
“Adhabu hii, itawahusu wafanyabiashara wenye kipato cha Sh 45,000 kwa siku sawa na Sh milioni 14 kwa mwaka, ambapo faini kwa wasiotumia mashine hiyo ni Sh milioni 3.
“Tumeleta watu 200,000 ambao watatumia mashine hizi lakini hadi sasa kuna wafanyabiashara asilimia 10 tu na TRA imeingia mkataba na wauzaji mashine 11 kila mkoa, hivyo ni wajibu wa wafanyabiashara kuhakikisha wanatumia mashine hiyo ili kuepuka usumbufu,” alisema Bateyunga.
Alisema licha ya kutoa elimu juu ya matumizi ya mashine hiyo, wafanyabiashara wengi wamekuwa wakijichanganya kuhusu kodi ya matumizi ya mashine hiyo wakifananisha na malipo ya ongezeko la thamani (VAT) na kusisitiza wafanyabiashara wengi walioingizwa katika mfumo wa VAT hawatoi risiti, jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Alisema matumizi ya mashine hizo, inasaidia kufahamu mauzo ya mfanyabiashara kwa mwaka mzima na kulipa kodi kulingana na mauzo yake. Aliongeza kuwa wauzaji wa mashine hizo wanatakiwa kuzitengeneza pindi zinapoharibika, hivyo ni muda muafaka wa wafanyabiashara wenyewe kumchagua muuzaji ambaye wao wanaona ni bora kwao.
Naye Meneja TRA Mkoa wa Ilala, Luvanda Ngoloka alisema kuanzia jana mamlaka hiyo imeanza msako kuwanasa wafanyabiashara wanaosafirisha mizigo na kukwepa kodi. Alisema TRA imebaini kuwa mizigo mingi inasafirishwa usiku kwa njia za panya na hadi sasa wamekamata mzigo wa tani tatu ambazo zimetelekezwa kutokana na kukwepa kodi.
“Maofisa wetu wapo nchi nzima, tutahakikisha tunakesha kwa kutembelea vituo vyote vya usafirishaji mizigo ili kuwanasa wanaokwepa kodi,” alisema Ngoloka. mwishio
EmoticonEmoticon