Nyamlani kuendeleza ya Tenga TFF




Mgombea Urais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF),Jumanne Nyamlani

Mgombea Urais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Jumanne Nyamlani amesema endapo atachaguliwa kuliongoza shirikisho hilo lenye mamlaka ya juu kisoka nchini, ataendeleza mambo yote mazuri yaliyofanywa na utawala unaoondoka madarakani chini ya Rais wa sasa, Leodegar Tenga.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Nyamlani ambaye kwa sasa ni makamu wa kwanza wa rais wa TFF, alisema uongozi wa Tenga (58), umefanya mambo mengi mazuri ambayo amepanga kuyaendeleza kwa maslahi ya soka la Tanzania.

"2004 Tenga aliingia madarakani kuchukua uongozi katika shirikisho lililokuwa 'limekufa'. TFF, kipindi hicho iliitwa FAT (Chama cha Soka Tanzania) ilikuwa na madeni, haikuwa na Katiba, lakini katika miaka nane ya uongozi wa Tenga hayo yote yamebaki kuwa historia," alisema Nyamlani na kuongeza:

"Tumeimarisha katiba, sasa tuna katiba bora ya TFF na tumekuwa wazi katika masuala ya mapato na matumizi ya fedha. Tuna kanuni za fedha ambazo hazikuwapo, TFF sasa ni taasisi kubwa yenye wafanyakazi wengi. Nakumbuka 2004 basi la FAT liliuzwa kwa sababu hatukuwa na fedha za kumlipa mmoja wa wafanyakazi wetu."

Nyamlani, ambaye 2008-2012 alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Dar es Salaam (DRFA), aliendelea kueleza kuwa katika kuhakikisha Tanzania inapiga hatua kisoka na kushinda mataji makubwa kwenye michuano ya kimataifa, atafanya kazi kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa).

Alisema ataanza na utekelezaji wa mpango wa maendeleo ya soka 2003-2006 na baadaye atajikita katika ahadi zake tisa kwa Watanzania ambazo ni kuimarisha usimamizi na menejimenti ya soka katika ngazi zote, kupiga vita rushwa katika soka, kukuza soka la watoto, vijana na wanawake, kuimarisha uwezo wa rasilimali fedha kwa shirikisho, kuongeza ubora na uwezo wa marefa, walimu na wataalam wa afya za michezo.

Zingine ni kuongeza ubora wa Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na ligi za wilaya na mikoa, kuongeza idadi ya mawakala wa wachezaji, kuimarisha ushirikiano wa TFF na serikali na kuwa na uhusiano mzuri na mashirikisho ya Kimataifa, CAF na Fifa.

"Nitaendeleza misingi ya utawala bora ambayo Tenga anatuachia.
Hatukuwa na kamati za kuwaadhibu watu wanaojihusisha na rusha kwenye soka. Tulikuwa tunalazimika kuwashirikisha Takukuru, lakini sasa vyombo hivyo vipo na tutakuwa tunawaadhibu mara moja na kwa haraka zaidi," alisema.

"Utulivu na uwazi uliojengwa na Tenga TFF umetusaidia kupata wadhamini wengi.
TBL wanatoa Sh. bilioni 3.5 kudhamini timu ya taifa. Azam TV nao wamejitokeza na kutoa fungu nono (Sh. bilioni 5.6) kudhamini matangazo ya Ligi Kuu. Ni kwa sababu ya utawala bora wa Tenga na uwazi tunaouonyesha TFF," aliongeza Nyamlani.

Uchaguzi Mkuu wa TFF, ambao ulitakiwa kufanyika Februari 24 mwaka huu kabla ya kusimamishwa na Fifa, utafanyika keshokutwa jijini Dar es Salaam huku Nyamlani akichuana na Mwenyekiti wa Chama cha Soka Kagera (KRFA), Jamal Malinzi kuwania kumrithi Tenga katika nafasi ya urais.
Previous
Next Post »