WAZIRI FEREJI AZINDUA BODI MPYA YA MAKAMISHNA WA TUME YA UKIMWI VISIWANI ZANZIBAR


DSC06234

Waziri  wa Nchi Afisi ya Makamu wa kwanza waRais Bi. Fatma Abdulhabib Fereji  akizindua bodi mpya ya Makamishna wa Tume ya Ukimwi Zanzibar kwenye ofisi ya Tume ya Ukimwi Shangani.
DSCF2467

Na Ramadhani Ali, Habari Maelezo Zanzibar                          
Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib Ferej leo amezindua Bodi mpya ya Makamishna wa Tume ya Ukimwi Zanzibar na kuitaka kushirikiana kwa karibu zaidi na wadau mbali mbali kuanzia ngazi ya chini ili kuhakikisha maambukizi ya janga la Ukimwi yanapungua na kufikia lengo la  Zanzibar bila Ukimwi inawezekana.
Waziri Ferji amewaeleza wajumbe hao kwamba Ukimwi ni janga la Taifa, na mapambano ya ya gonjwa hilo yamejaa changamoto nyingi ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi kwani  bado wapo watu hawataki kuelewa ingawa juhudi kubwa za kuwaelimisha zimechukuliwa.
Katika kuanza kazi zake, Waziri wa Nchi Afisi ya Mkamu wa Kwanza wa Rais ameieitaka safu  mpya ya Makamishna  kufanya ziara za mara kwa mara sio katika maofisi tu bali  kuwapitia wadau kujua changamoto zinazowakabili kwa lengo la kunagalia namna Tume inavyoweza kusaidiana nazo katika kuzitatua.
“Hilo  ni jambo muhimu sana na tukifanya hivyo tutaweza sote kujiridhisha na yale tunayojipangia kuyatekeleza katika mipango yetu ya mwaka au robo mwaka,”alisisitiza Waziri Fatma Abdulhabib Ferej.
Amewashauri Makamishna  wapya  katika kipindi  cha miaka mitatu ya kazi, kuendelea kuwa karibu zaidi na watendaji  na Wafanyakazi wa Tume katika kusimamia  utendaji na uwajibikaji ili kufikia lengo  la kuanzishwa sheria namba 3 ya mwaka 2002 ya  Tume ya Ukimwi Zanzibar.
Amesema kwa upande wake na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwa jumla wapo tayari kutoa kila msaada kwa Tume kila itapohitajika ili kufanikisha kazi zao kwa ufanisi mkubwa.
Ameeleza matumaini yake kuwa kutokana na Tume hiyo mpya kusheheni Makamishna wenye uzoefu mkubwa na shughuli  za Bodi na mapambano dhidi ya ukimwi  hategemei kama shughuli zitazozorota.
Amewapongeza wajumbe  waliomaliza muda wao kwa namna walivyoisaidia Tume ya Ukimwi licha ya changamoto nyingi walizokabiliana nazo lakini busara zao na uwezo wao umesaidia sana ufanisi katika shughuli za Tume.
‘Ni imani yangu ya dhati  kwamba mafanikio yaliyopatikana ndani ya Tume yametokana na michango yao kutokana na uzoefu wao pamoja na maelekezo yao, ’alisema Waziri Ferej.
Alitaja moja  ya fanikio la kujivunia kwa Makamishna hao ambalo ni la kupigiwa mfano ni kwamba wakati baadhi ya nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara wamefikia kiwango cha maambukizo cha asilimia kati ya ishirini na thelathini katika miaka ya hivi karibuni, Zanzibar imeweza kudhibiti kiwango cha maambukizo chini ya asilimia moja.

Amewaomba wajumbe hao kuwa tayari kuendelea kuisaida Tume mpya kila watakapohitajiwa kufanya hivyo kwa vile ni watu wenye uwezo mkubwa katika kusaidia maendeleo ya Tume ya Ukimwi.
Katika uzinduzi wa Bodi uliofanyika Tume ya Ukimwi Shangani, limpongeza Mwenyekiti aliemaliza muda wake Professa Saleh Idrissa Mohammed kwa kuteuliwa tena na Rais kwa kipindi chengine  cha miaka mitatu na kueleza kuwa ni kutokana na uwezo wake mkubwa alioonyesha katika kuiongoza Bodi hiyo.
Kwa upande wake Professa Idrissa amemuhakikishi Waziri kwamba watatekeleza wajibu wao waliokabidhiwa na Taif na kuhakikisha huduma za Tume zinawafikia wananchi wote na kufikia lengo la kuhakikisha janga la ukimwi linapungua kwa kiasi kikubwa na vizazi vijavyo visome historia kuwa kulikuwa na Ukimwi Zanzibar.
Makamishna  wapya wa Tume ya Ukimwi Zanzibar ni Abeid Saad Said kutoka Taasisi zisizo za Kiserikali, Sheikh Mziwanda Ahmed Taasisi za Dini, Hasina Hamad kutoka vyombo vya Habari, Munira Humud Taasisi za Biashara na mjumbe mmoja kutoka Jumuiya ya watu wanaoishi na Viruza vya ukimwi Zanzibar.
Wajumbe  wanaoingi moja kwa moja kwa mujibu wa nyadhifa zao ni Makatibu Wakuu wa Wizara ya Elimu, Wizara ya Afya, Wizara ya Vijana, Wanawake na watoto na Uwezeshaji wananchi kiuchumi pamoja na Wizara ya Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ.
Previous
Next Post »