POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kukutwa na maiti, iliyokuwa na pipi 33 za dawa za kulevya aina ya heroin tumboni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi, Suleiman Kova alitaja waliokamatwa kuwa ni Nasri Omari (36), maarufu kama Rajabu Robot na Mwanaisha Salim( 36), mkazi wa Kigogo Luhanga.
“Kila pipi ina urefu wa sentimita sita...tulipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa huko Tabata kuna mtu mmoja alifariki ghafla muda mfupi baada ya kutoka bafuni kuoga na tukaamua kulifuatilia tukio hilo” alisema.
Alisema makachero walifika eneo la tukio, nyumbani kwa Omari na kuhoji hatimaye kugundua uwepo wa maiti sebuleni ikiwa imelazwa chali katika godoro sakafuni huku akiwa hana nguo na amefunikwa na shuka.
“Omari ambaye ndiye mmiliki wa chumba kilichokutwa maiti, alisema marehemu anajulikana kwa jila la Rajabu Kandunda (43), maarufu kama Mashaka Mabruki” alisema.
Kamishna Kova alisema uchunguzi wa awali, ulionesha kuwa Kandunda alifika kutoka Mtwara Septemba 21 kwa maelezo kwamba alikuwa mgonjwa na alikwenda kuchukuliwa na watuhumiwa hao wawili.
Alisema uchunguzi huo, ulifanywa na jopo la madaktari wawili na kushuhudiwa na maofisa wa juu wa Polisi na ndugu wa karibu wa marehemu, ambapo katika uchunguzi huo wa mwili wa marehemu, tumboni zilikutwa pipi 33 za dawa za kulevya aina ya heroin, zenye thamani ya mamilioni ya fedha.
“Zipo taarifa zinazoonesha kwamba alikuwa ni mhalifu mzoefu wa usafirishaji wa dawa za kulevya, kwani kabla ya kurudi Tanzania alikuwa akitumikia kifungo nje ya nchi barani Asia” alisema.
Kova alisema uchunguzi zaidi unafanyika ili kujua mtandao mzima wa usafirishaji wa dawa hizo, ambao umemhusisha marehemu. Alisema wote watakaobainika kuhusika, watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha alisema baada ya upekuzi, marehemu huyo alikutwa na vielelezo vingine, ikiwemo fedha za Kenya Sh 700, Dola za Marekani 100 na fedha ya Ushelisheli.Alisema operesheni ya kukamata dawa za kulevya, inaendelea. Aliomba raia wema kuendelea kutoa taarifa za dawa hizo, kwani zina madhara makubwa kwa wananchi, hasa vijana.
EmoticonEmoticon