WASOMI WAMCHAMBUA BALOZI WA CHINA


balozipx1 d2a26
WAKATI vyama vya upinzani nchini vikipinga kitendo cha Balozi wa China nchini, Dk. Lu Younqing, kupanda jukwaani katika mkutano wa hadhara wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), uliofanyika mkoani Shinyanga, hivi karibuni, baadhi ya wasomi nchini nao wamejitosa katika mjadala huo. 
Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Azaveri Lwaitama, alisema kitendo kilichofanywa na balozi huyo hakiwezi kukubalika kwa kuwa kinaonyesha ana upendeleo wa chama kimoja.
Kutokana na hali hiyo, alisema kuna haja Serikali ifanye jitihada za kumuondoa balozi huyo nchini, kwa kuwa kitendo cha kuendelea kumwacha kitakidhoofisha CCM.
"Kama hataondolewa nchini, wapinzani nao wataweza kulipa kisasi kwa kuwatumia mabalozi kadhaa kwa kisingizio, kwamba CCM nao wamefanya.
"Lakini tuelewe kwamba, ni makosa kwa balozi yeyote kujihusisha na siasa na kushabikia chama fulani tena jukwaani kama alivyofanya balozi huyo wa China.
"Sote tunafahamu uhusiano wetu na China na jinsi mataifa mbalimbali yanavyoshirikiana na vyama vya siasa, chama tawala pia kina chama chao kinachoshirikiana nao katika mataifa mengine.
"Lakini, chama tawala katika nchi yoyote kinachoshirikiana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR-Mageuzi au Chama cha Wananchi (CUF), balozi wake angefanya kama alivyofanya Younqing, tayari ungeshasikia balozi huyo amesharudishwa nchini kwao.
"Katika hili naamini kama hatua hazitachukuliwa, wapinzani na mabalozi wengine wanaweza wakafanya na wakiulizwa watasema mbona yule na hatua hazikuchukuliwa?
"Suala la ushabiki wa vyama halizuiliki, kwa sababu mabalozi wengi wanavishabikia, lakini wanafanya kimya kimya wakiwa wanakunywa chai huko, si hadharani kama alivyofanya huyo," alisema Dk. Lwaitama.
Kwa upande wake, Mhadhiri mwingine wa UDSM, Dk. Bashiru Ally, alisema Watanzania waache kutafsiri sheria kwa mtazamo finyu kwani sheria hizo na siasa wanazoziita za kimataifa, ziko kwa maslahi ya watu fulani.
Alisema hata kama balozi huyo amevunja sheria, hatakuwa wa kwanza na hakuna haja ya kupoteza muda kumjadili.
"Anayetafsiri sheria kimbumbumbu naye ni mbumbumbu, sheria na siasa za kimataifa ziko kwa ajili ya maslahi ya watu wengine, ndiyo maana Marekani ilipochangia kuuawa kwa Rais wa Libya, hatukusikia maneno maneno.
"China imewahi kuvamia nchi gani, imewahi kumuuzia nani silaha, sasa utasemaje huyu amevunja sheria ya kimataifa wakati anazungumzia bei ya pamba kama sehemu ya kuangalia fursa ya uwekezaji?
"Pamba inalimwa na wakulima, si CCM, tuache kutafsiri sheria hizi kimbumbumbu, tujiulize zimetungwa na nani, zinasimamiwa na nani na kwa maslahi ya nani, sheria ya kipuuzi tu hiyo.
"Binafsi namsifu balozi, labda jambo la kujadili ni je, aliyoahidi pale atatekeleza na yatatunufaisha?" alisema Dk. Bashiru.
Naye, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, UDSM, Dk. Benson Bana, alisema, mkataba wa Viena anaodaiwa kuuvunja balozi huyo uko wazi na kwamba haujataja mambo ya siasa na mwenye dhamana ya jambo hilo ni Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wala si chama cha siasa.
"Hii si kazi ya chama cha siasa wala msajili wa vyama kuzungumzia suala hili, lakini angalau msajili alikionya CCM pekee.
"Wizara ya Mambo ya Nje ambao ndiyo wenye dhamana, wanajua cha kufanya, wana jinsi yao ya kuonya kidiplomasia.
"Lakini jambo la msingi hapa, waangalie mkataba unasema nini kisha balozi akumbushwe wajibu wake, si kumtisha," alisema Dk. Bana.
Wakati wasomi hao wakisema hayo, aliyekuwa Askofu wa Kanisa la Anglikana nchini, Dk. Valentino Mokiwa, alionekana kumtetea balozi huyo kwa kusema kuwa Watanzania wanatakiwa kuelewa, kwamba balozi huyo hakwenda kwenye shughuli za kampeni bali katika masuala ya kukuza uchumi.
"Tuisaidie nchi yetu isiwe inashughulika na vitu vidogo vidogo, Watanzania tuna ugonjwa huo, CCM kumwalika balozi yule si dhambi, naomba asitishwe na mwishowe akaiona Tanzania si nchi ya amani.
"Hii nchi ina matatizo mengi ya kufanyiwa kazi, tusitafute namna ya kuharibu uhusiano wetu mzuri uliopo na China," alisema Dk. Mokiwa.
Naye, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Deus Kibamba, alisema hatua zilizochuliwa na Serikali ya Tanzania kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa dhidi ya balozi huyo, bado hazijitoshelezi.
Alisema kwamba, njia pekee ya kurudisha imani kwa Watanzania juu ya ubalozi wa China, ni kumrudisha kwao balozi huyo na kumleta mwingine atakayefanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi za kimataifa.
"Balozi Youqing amepoteza sifa za kuendelea kuwapo nchini, kwa sababu amevunja Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 ibara ya 41 (1-3) ambao unasimamia sheria za nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN).
"Kitendo hiki kimewafanya Watanzania kuwa na maswali, kwanza anaonekana ana uelewa mdogo juu ya uwakilishi wake au ana ajenda fulani ambayo ameipanga pamoja na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
"Ingawa msajili ameikemea CCM, onyo hilo ni dhaifu kwa sababu bado inaonekana chama na viongozi wake hawajutii walichokifanya, msajili alipaswa awatake Katibu Mkuu, Abdulrahaman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye waombe radhi.
"Pia Serikali ya Tanzania inapaswa kuiandikia Serikali ya China kuonyesha nia ya kumuondoa balozi wao nchini na kumleta mwingine ili kulinda uhusiano wetu uliodumu tangu uhuru," alisema Kibamba.

 Source: Mtanzania
Previous
Next Post »