Mbowe, Mbatia, Profesa Lipumba wamvaa IGP



Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Said Mwema (kulia) akiagana na Wenyeviti wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF (kushoto)Freeman Mbowe wa Chadema (wapili kulia) na James Mbatia wa NCCR-Mageuzi, jijini Dar es Salaam jana.

 Vyama vya siasa vya upinzani vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, leo vitafanya mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Jangwani kuhamasisha wananchi wapinge kile wanachodai ni hujuma dhidi ya Mchakato wa Katiba Mpya.
Hatua ya kufanya mkutano huo, ilifikiwa jana baada ya wenyeviti wa vyama hivyo kumvamia Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema ofisini kwake wakipinga kitendo cha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam kupiga marufuku maandamano waliyokuwa wayafanye leo jijini humo.
Katika mkutano wao na IGP Mwema, viongozi hao walikubaliana maandamano hayo yasitishwe kwa sababu za kiusalama, lakini wafanye mkutano huo wa hadhara.
Wenyeviti hao wa vyama vya Upinzani, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi, Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), ambao walikutana na Mwema jana mchana.
Hatua ya viongozi hao ilitokana na tamko lililotolewa juzi na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, Suleiman Kova kusitisha maandamano ya vyama hivyo yasifanyike.
Kova alitaja sababu za uamuzi huo kuwa ni kuhofia yatasababisha kusitishwa kwa shughuli za kiuchumi pamoja na kuwepo taarifa za kiintelijensia kwamba yatakuwa na vurugu.
Tamko hilo liliwakera viongozi wa vyama hivyo vitatu vilivyotangaza kushirikiana katika kupinga kile wanachodai ni uporaji wa haki ya wananchi kutunga Katiba yao.
Mazungumzo wenyeviti hao na IGP yalianza saa 6 mchana na kumalizika saa 11 jioni, ambapo walitoa taarifa ya pamoja kuhusu waliyokubaliana.
Akitangulia kutoa taarifa hiyo, kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba alisema: “Tumekubaliana kesho tutafanya mkutano Viwanja vya Jangwani. Tumekubaliana kusitisha maandamano hadi Oktoba 5, (mwaka huu).”
Aliongeza kuwa wamekubaliana pia kwamba watafanya mkutano mwingine wa hadhara Visiwani Zanzibar, Jumatano ijayo.
Hata hivyo, katika taarifa ya pamoja, ulitokea kuhitilafiana kwa kauli, pale IGP Mwema alipokuwa akitoa ya upande wake.
Hali hiyo ilitokana na kauli ya Profesa Lipumba kusisitiza kuwa mikutano na maandamano ni haki ya msingi kwa vyama vya siasa na kwamba wanachopaswa ni kutoa taarifa kwa polisi na wala siyo kuomba kibali.

Previous
Next Post »