Siku moja baada ya kutangazwa rasmi
kwamba aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa
amestaafu kwa mujibu wa sheria, amejitokeza na kueleza yaliyo moyoni
mwake.Katika mahojiano maalumu na Mwananchi jijini Harare jana, Tendwa
alisema amepokea kwa mikono miwili kustaafu kutoka katika nafasi hiyo
nyeti katika siasa za Tanzania, huku akisema anajiona mwenye bahati
kufanya kazi na marais wawili katika nafasi yake.
Tendwa amefanya kazi chini ya uongozi
wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na baadaye Rais Jakaya Kikwete. Nafasi ya
Tendwa, imechukuliwa na Jaji Francis Mutungi ambaye alikuwa jaji wa
Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma.
Akizungumzia kuhusu viongozi wa vyama
vya upinzani kupokea kwa nderemo kustaafu kwake, Tendwa alisema wala
hashangai kuyasikia hayo kwani inaonyesha kwamba kazi yake alikuwa
akiifanya vyema na mujibu wa sheria.
"Unajua unapokuwa msajili na ukaona
wadau wote wanakushangilia hapo ujue kuna tatizo kubwa, nimekuwa
ninafanya kazi yangu vizuri sana kwa kuzingatia misingi ya sheria ambayo
imewekwa kwa mujibu wa sheria na kanuni,"alisema Tendwa.
Alisema kwamba, "Unajua kuvilea vyama
ni kazi kubwa sana ndugu yangu, maana kuna wakati hata Chama Cha
Mapinduzi (CCM) walikuwa wanasema ninaegemea na kuvipendelea sana vyama
vya upinzani. Leo nimestaafu nasikia vyama vya upinzani vinasema kwamba
nilikuwa nawapendelea CCM, hiyo inaonyesha kwamba nilikuwa ninafanya
kazi yangu sawa sawa."
Kitu gani ambacho Tendwa hatakisahau?
Alisema kwamba katika miaka yake 13 ambayo amekuwa msajili hatomsahau waziri mmoja wa CCM.
Hata hivyo, Mwananchi lilimbana
kumtaja waziri huyo, lakini agoma kwa madai kwamba hapendi kuendeleza
malumbano naye baada ya kustafu kwake utumishi wa umma.
Tendwa alisema katika utumishi wake, waziri huyo alikuwa akimpatia wakati mgumu sana kwa kumpakazia kwamba yeye ni mpinzani.
"Katika miaka yangu 13 ofisini
sitaweza kumsahau huyo waziri maana alikuwa ananipakazia kwamba mimi ni
mfuasi wa vyama vya upinzani. Ninamshukuru Mungu kwamba baadaye alikuja
kuniomba msamaha, lakini ilikuwa imenisumbua sana katika kazi zangu,"
alisema huku akionyesha masikitiko
Kwa nini vyama vinashuka?
Kuhusu kushuka na kupanda kwa vyama
vya siasa hasa vile vya upinzani nchini baada ya uchaguzi kumalizika,
Tendwa alisema katika kipindi chake cha uongozi aligundua kuwa migogoro
ndani ya vyama hivyo ndio chanzo kikubwa cha kupoteza mvuto kwa
wananchi.
"Tatizo la vyama vingi vya upinzani
Tanzania vinadhani kuwapata wabunge basi ndio vinakuwa vimechukua
Serikali, vinasahau kujizatiti na kujipambanua mbele ya macho ya
wapigakura kuwa vinasimamia kitu gani, badala yake nimekuwa vikiishia
kwenye migogoro isiyo ya lazima," alisema Tendwa.
Tendwa alielezea jinsi ambavyo
NCCR-Mageuzi ilivyokuwa na nguvu sana katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
1995, lakini baada ya kuingia kwenye migogoro chama hicho kikapoteza
mvuto.
"Badala ya kujiingiza kwenye migogoro vinatakiwa kujipanga kisayansi, lazima wajue kwamba siasa ni sanyasi," alisema.
Alisema hata CUF kilianza kupoteza mvuto kwa jamii baada ya kupata wabunge na kuanza kuibuka migogoro ya ndani.
Jambo la kujivunia
Tendwa alisema anajivunia kitengeneza muundo wa ofisi ambayo inazingatia maadili.
Alisema wakati anakabidhiwa ofisi
alikuwa peke yake ndiye mwanasheria mwenye kiwango cha shahada ya chuo
kikuu, lakini hivi sasa msajili mteule atakuta zaidi ya wanasheria 16
katika ofisi zote tano za kanda pamoja na makao makuu.
Pia alisema aliweza kuleta nidhamu ya
matumizi ya fedha pamoja na kuleta weledi katika kujenga misingi imara
ya ofisi hiyo ambayo imekabidhiwa jukumu kuvisimamia na kuvilea vyama
vya siasa nchini.
Ushauri kwa mrithi wake
Tendwa alisema hawezi kumfundisha kazi
Jaji Mutungi kwani anaamini atafanya kazi yake kwa mujibu wa sheria na
taratibu kama ambavyo miongozo inavyotaka.
"Mutungi atafanya kazi kwa mujibu wa
sheria, siku zote atafuata sheria na kutafsiri sheria maana yeye ni
Jaji. Ninawaomba wadau wampatie ushirikiano maana sasa anakuja kufanya
kazi na wanasiasa," alisema Tendwa.
Alisema endapo Jaji Mutungi ataanza kubezwa na wanasiasa anatakiwa kujua ndani ya moyo wake kwamba anafanya kazi yake sawasawa.
"Ila kama ataona wanasiasa wanamsifia
basi atakuwa kuna sehemu ambazo hatekelezi vyema majukumu yake. Kufanya
kazi na wanasiasa kunahitaji busara na sio kufuata vitabu vya sheria
vinasemaje," alimshauri Jaji Mutungi.
Alisema baada ya kustaafu ana mpango wa kufanya kazi za ushauri katika siasa za kimataifa na sio siasa za maji taka.
"Nahitaji muda kidogo kufikiri
nitafanya nini ila napenda sana kuwa 'international consultant' kwenye
masuala ya siasa, lakini pia ikumbukwe kwamba mimi ni mwanasheria ambaye
nimekuwa katika masuala ya uwakili kwa takriban miaka 23. Muda utaongea
nifanye nini, ngoja kwanza nikabidhi ofisi," alisema Tendwa.
Chanzo:Mwananchi
EmoticonEmoticon