Kauli ya Julius S. Mtatiro kuhusu tukio la sheikh Ponda kupigwa risasi mjini Morogoro

Muda si mrefu nimetoka kuongea na shuhuda mmoja aliyekuwepo Morogoro. Ni kweli kuwa Sheikh PONDA amejeruhiwa vibaya kwa RISASI.
Huu ni mwendelezo wa matukio ya kuwawinda viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, waandishi wa habari na wanaharakati ambao serikali inaamini ni “watu hatari”.

Hivi karibuni, taarifa za ndani za serikali zimekuwa zikimuonesha Sheikh Ponda kama “mtu hatari kwa usalama wa taifa”, huu ni upuuzi na ujinga mkuu ambao utatupeleka pabaya.
Ikiwa kuna mtu ni hatari sana kwa taifa, na serikali ina ushahidi, kwa nini isimfungulie mashtaka mtu huyo na ipeleke ushahidi huo mahakamani ili mahakama ipime na kuamua au la!

Serikali inayotumia “approach” (mbinu) ya kushambulia, kujeruhi kwa nia ya kuwaua watu wenye msimamo tofauti na serikali hiyo, hii inakuwa “serikali hatari, ya kijinga, dhaifu na iliyoshindwa kuongoza”, serikali ya namna hii “is more dangerous to the peace of the nation than the dangerous persons themselves” (serikali ya namna hii ni serikali hatari mno kwa amani ya taifa kuliko watu inaowadhania kuwa hatari”.

Mimi nachojua, Sheikh Ponda ni mwanaharakati wa kiislamu anayebeba matumaini, hoja na visheni ya waislamu walio wengi. Kwa upande mwingine serikali ya CCM inamuona Sheikh PONDA kama mtu hatari kwa sababu hoja na visheni zake vikifanikiwa vitawatoa waislamu chini ya BAKWATA ambayo inatumiwa na serikali ya CCM kama nyenzo ya kuwadhibiti waislamu katika masuala yao ya msingi na hata baadhi ya haki zao muhimu za kiimani.

Serikali yoyote ya kipuuzi na iliyokufa “a failed state” haifikiri namna ya kutafakari hoja zinazokinzana na serikali na kuzitafutia ufumbuzi mezani. Hufikiri kutumia nguvu, kuwatisha watoa hoja husika na hata kuwaua pale nafasi inapopatikana, ilimradi udhibiti “sensorship” uendelee.

Serikali mfu kama ya CCM huwasha kiberiti yenyewe na baadaye huhaha kuzima moto ikiwalaumu watu wengine kwa matatizo yaliyoanzishwa na serikali yenyewe.
Ikiwa viongozi tutachekelea unyama huu na kuacha fulani atambuliwe kama “mtu hatari sana” ATI kwa sababu tu yeye ni dini fulani, ni kweli mhusika atashughulikiwa ipasavyo, atateswa tutachekelea, ataumizwa tutasheherekea na atauawa tutapiga nderemo na vifijo.

Serikali mfu haitaishia hapo, ikimaliza kumshughulikia yeye kwa dini yake itahamia kwako, itakuita “mtu hatari sana” kwa sababu ya chama chako, kwa sababu ya uanaharakati wako, kwa sababu ya uandishi wako na kwa sababu ya msimamo na mtizamo wako ambao unapingana na serikali. Nani atabaki salama?
Mwalimu Nyerere aliwahi kusema, “ukinywa damu ya mtu, utaendelea kunywa tu”. Nami nasema, tukichekelea na kukubali propaganda za CCM kuwa

Sheikh Ponda ni mtu hatari sana, akishamalizwa watahamia kwetu(kwangu na kwako), mimi na wewe tutapewa “uhatari” na tutasakwa kwa mtutu wa bunduki tuuawe haraka ili taifa libaki kuwa salama.
Serikali ya CCM iache mbinu hizi ambazo tulishazijua.

Serikali ikatatue tatizo la msingi la MZOZO WA MIONGO KADHAA KATI YAKE NA WAISLAMU. CCM iwaache waislamu watafute uongozi wao huru kabisa, wanaouamini. Kufikiri ATI maoni ya waislamu yataendelea kusimamiwa, kuratibiwa na kuongozwa na BAKWATA ni kupoteza muda na kijidanganya. Mbona sisi wakristu tuna taasisi zetu muhimu na imara za kidini na tunaziamini? Kwa nini serikali ya CCM inaendelea kuwashika waislamu na kuwadhibiti kwa kuitumia taasisi ambayo waislamu hawaiamini?

Jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa, pamekuwa na marais wawili ambao ni waumini wa dini ya kiislamu, Mzee Mwinyi na sasa Mhe. Kikwete, hawa ni waislamu kabisa, ina maana hawajui malalamiko ya waislamu ya miaka nenda rudi? Kama Kikwete na wenzie walichoshwa na mauaji yaliyokuwa yanaendelea Zanzibar na wakaamua kuwaacha wazanzibari waamue hatima yao na Leo imeundwa SUK. Kina Kikwete haohao wanashindwaje kusema matatizo ya waislamu sasa basi na wakawaachia waislamu huru waamue hatima yao, wawe na vyombo wanavyoviamini visimamie maslahi yao. Mwinyi na sasa Kikwete siyo waislamu? CCM ina maslahi gani BAKWATA?

Mtizamo wangu pia ni kwamba, waislamu wanaweza kuwa wanamalizana wao kwa wao bila kujua.
Pale Marekani kulikuwa na tatizo la msingi kwa wamarekani wengi wa kipato cha chini, huduma za afya zilikuwa kuzungumkuti. Sehemu kubwa ya waathirika wa jambo hili walikuwa wamarekani weusi. Marais wote wazungu waliopita hawakuwahi kufikiri kulitatua, alipopata nafasi Obama akalibainisha Suala la afya kwa wamarekani wa kipato cha chini kama tatizo la msingi linalohitaji utatuzi wa haraka. Obama akatengeneza muswada wa bima ya afya, akambana hadi ukawa sheria, Leo wamarekani wa kipato cha chini ambao wengi ni weusi wanafaidika na mpango huo. Obama alipigwa vijembe kuwa analeta muswada wa kuwapendelea watu weusi lakini aliwapuuza wapinzani wake, alijua anafanya jambo ambalo litaondoa mgawanyiko na ukosefu wa haki muhimu ambalo lingeisumbua Marekani ya baadaye.

Hapa kwetu tuna marais wanaonea haya dini zao na wanashindwa kutatua matatizo ya msingi ya kundi ambalo wameliishi na kuonja adha ya kero zao.

Kuwaacha waislamu wajichagulie vyombo huru vya kujiongoza ni kuongeza na kupanua wigo wa demokrasia na uhuru muhimu kwa watanzania wote, hili halitakuwa na faida kwa waislamu peke yao, lina faida kwa nchi nzima. Ni bora rais uitwe mdini kwa kuondoa udhibiti wa chama chako kwa taasisi ya kidini na kuiacha huru kuliko kuacha mifarakano na malalamiko ya kundi linalodhaniwa linaonewa kwa miongo kadhaa yaendelee.




Mimi nadhani waislamu wana matatizo ya msingi kati yao, panahitajika viongozi imara wanaoliona hilo. Ikiwa yataachwa au kushughulikiwa kwa mtindo huu wa kuvizia na kupiga RISASI wale wanaotetea maslahi halisi ya waislamu, hayatakwisha.
Ikiwa atauawa Ponda mmoja eti kwa sababu anadhaniwa kuwa “mtu hatari”, in the next morning watazaliwa Ponda wengine hatari zaidi wapatao 1000.


Uhuru wa Dokta hauzimwi kwa RISASI.
Sote bila kujali itikadi zetu za kidini, kisiasa na kimtizamo, TULAANI KWA NGUVU UNYAMA ALIOFANYIWA SHEIKH PONDA.
Julius Mtatiro,
+255717536759.
Maoni haya ni yangu binafsi, yasihusishwe na chama changu wala nafasi yangu ya uongozi ndani ya chama.
Previous
Next Post »