MCHEZAJI WA ZAMANI WA YANGA NA STARS BARAKA KITENGE AMBAYE NI BABA WA MTANGAZAJI MAULID KITENGE AFARIKI DUNIA

 

 MAULID KITENGE WA ITV MTOTO WA MAREHEMU BARAKA KITENGE

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko habari ya kifo cha mchezaji wa zamani wa timu ya Yanga na Taifa Stars, Baraka Maulid Kitenge (74) kilichotokea jana mchana, jijini Dar es Salaam.

Ofisa Habari wa Shirikishi hilo, Boniface Wambura, alisema jana kuwa, Kitenge, baba wa mtangazaji wa Radio One na ITV, Maulid Kitenge, akiwa mchezaji alitoa mchango mkubwa katika soka ya Tanzania.

“Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa soka kwani nyakati tofauti, Kitenge akiwa mchezaji, alitoa mchango mkubwa katika timu alizochezea, mchango wake utakumbukwa daima,” alisema Wambura.

Alisema Kitenge amepoteza maisha akiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa amelazwa akisumbuliwa na kansa ya uti wa mgongo.

Wambura alisema akiwa na wachezaji wengine kama Athuman Kilambo na Abdulrahman Juma, walikuwa chachu ya mafanikio ya Stars.

Wambura alisema TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu, Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na Klabu ya Yanga na kuwasihi kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Kuhusu mazishi, alisema mipango inafanywa nyumbani kwa marehemu, Yombo Vituka (Jet), jijini Dar es Salaam. Mungu aiweke roho ya marehemu Kitenge mahali pema peponi. Amina.

 

Previous
Next Post »