Tumeshangazwa mno na ukimya wa Serikali kuhusu
janga kubwa la biashara ya dawa za kulevya ambalo limeikumba nchi yetu
kwa muda mrefu sasa. Hatutaki kuamini kwamba Serikali haina taarifa za
kuwapo kwa janga hilo hapa nchini, wala kuamini kwamba Serikali hiyo
bado haijatambua ukubwa wa tatizo hilo.
Mbali na kauli nyepesi za polisi na taasisi
nyingine husika kwamba zinafanya uchunguzi ili kugundua watu
wanaojihusisha na biashara hiyo, hatujasikia kauli nzito kutoka kwa
kiongozi mkuu wa nchi, Rais Jakaya Kikwete ambaye ndiye pekee mwenye
sauti yenye mamlaka anayeweza kuzungumzia tatizo hilo, hasa kwa kutilia
maanani kwamba biashara hiyo haramu sasa imefikia kiwango cha kutisha na
wananchi wamechoka kusikia ahadi zisizotekelezeka za kuikomesha.
Hivyo, wakati huu wananchi hawategemei Rais
Kikwete atoe kauli zilizozoeleka kwamba anayo orodha ya watu
wanaojihusisha na biashara hiyo na kuwataka waache uhalifu haraka.
Tunasema kauli kama hizo zimezoeleka kwa wananchi na sasa ni wakati wa
kuwaeleza hatua zilizochukuliwa dhidi ya watu hao, ikiwa ni pamoja na
mipango na mikakati inayochukuliwa na Serikali hivi sasa katika
kutokomeza janga la dawa za kulevya hapa nchini.
Yamesemwa mengi kuhusu nguvu ya kifedha waliyonayo
magwiji wanaoendesha biashara hiyo, kwamba wanajigamba hadharani kwamba
wameitia Serikali yetu mfukoni. Pamoja na majigambo hayo, sisi
tunadhani kwamba kinachohitajika kwa sasa ni Rais Kikwete kuthibitisha
kwa vitendo kwamba kweli anao ujasiri na utashi wa kisiasa wa kutokomeza
biashara hiyo ambayo tayari imevuruga maisha ya vijana wengi hapa
nchini na kuharibu taswira ya nchi yetu.
Hatuna shaka yoyote kwamba Rais anazo zana zote za
kupambana na watu hao kwa kuwa yeye kikatiba ndiye mkuu wa nchi,
kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu, kwa maana ya kuwa kamanda wa
majeshi ya ulinzi na usalama. Kwa nafasi hiyo, anawezaje kushindwa vita
ya kutokomeza biashara hiyo kama anao ujasiri na utashi wa kisiasa wa
kushinda vita hiyo, huku wananchi kwa ujumla wao wakiwa nyuma yake?
Wananchi wanauliza maswali kuhusu wapi Rais
Kikwete amekwazwa katika vita hiyo. Maswali hayo ni ya msingi, kwani sio
siri kwamba hivi sasa zipo taarifa za kutosha kuhusu mitandao ya
biashara hiyo na majina ya magwiji wanaomiliki na kuendesha biashara
hiyo.
Serikali inajua fika kwamba mtambo wa kuongeza
thamani ya heroini umeingizwa nchini. Kilo 150 za heroini walizokamatwa
nazo wasichana wawili wa Tanzania walipotua huko Afrika ya Kusini hivi
karibuni zilitengenezwa na mtambo huo.
Serikali inajua kwamba wapo maelfu ya Watanzania
walio katika magereza katika nchi mbalimbali duniani baada ya kubambwa
na dawa za kulevya. Baadhi yao tayari wametaja majina ya magwiji wa
biashara hiyo na kinachotakiwa sasa sio tu Serikali kuyafanyia kazi
majina hayo, bali kuwafuata vijana walio katika magereza huko nje ili
kupata taarifa za kina kuhusu mitandao hiyo.
Ukimya wa Serikali unatia shaka. Sasa yanahitajika
mabadiliko makubwa katika uongozi wa viwanja vyetu vya ndege, vikosi
vya ulinzi na usalama na mamlaka za kupambana na dawa za kulevya. Sisi
tunadhani mpango wa Serikali kutaka kubadilishana wafungwa na nchi
nyingine una ajenda ya siri, haufai.
Source:MWANANCHI
EmoticonEmoticon