WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta (pichani), amesema
litakuwa jambo la kuchekesha duniani iwapo nchi maskini kama Tanzania
itakuwa na marais watatu kama muundo wa serikali tatu uliopendekezwa
kwenye rasimu ya katiba mpya utapitishwa.
Vile vile, amesema licha ya kuwa kichekesho, muundo wa muungano ambao
utatengeneza marais watatu utasababisha gharama kubwa za uendeshaji na
kuwa mzigo mkubwa kwa uchumi. Aliyasema hayo jana wakati akifung
ua
mkutano wa siku tatu wa Baraza la Taifa la Vijana la Rasimu ya Katiba
mpya unaoendelea jijini Dar es Salaam.
Alisema inawezekana kabisa Tanzania ikawa na serikali tatu lakini wakati
huo huo ikawa na rais mmoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
wengine wakapewa majina mengine kama Makamu wa Rais ama Waziri Mkuu.
Sitta alisema kimsingi hapingi muundo wa serikali tatu bali anachopinga
ni utitiri wa marais unaoweza kutokea ambao utasababisha gharama kubwa
za uendeshaji wa serikali.
“Hebu fikiria tunakuwa na marais watatu, Rais wa Zanzibar anasafiri
kwenda nje, Rais wa Jamhuri ya Muungano naye anasafiri, Rais wa
Tanganyika naye anakwenda nje ya nchi, hivi huko nje si watatushangaa na
kutuona kioja jamani nchi maskini inafanya hivi,” alisema.
Aidha, Sitta alisema inawezekana kuwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na wale watakaoongoza Zanzibar na Tanganyika wakapewa nafasi
kama za Makamu wa Rais, Naibu Rais ama Waziri Mkuu.
Sitta alisema watu wanaopigia debe utitiri wa marais ni wale wenye uroho
wa madaraka ambao wanadhani inaweza kuwa njia rahisi kwao kufikia
malengo yao ya kisiasa.
“Mimi nadhani huu ni ubinafsi wa hali ya juu, kila mtu nchi hii anataka
kuitwa mheshimiwa rais, mimi nashauri kama muundo wa serikali tatu
utapitishwa basi tuwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hao
wengine watafutiwe majina mengine,” alisema Sitta.
Aliendelea kusema kuwa Watanzania wanapaswa kusimama kidete kuhakikisha
Katiba ijayo haitengenezi rais wala serikali dikteta ili nchi iende kwa
misingi ya demokrasia na utawala bora.
Alisema Katiba mpya lazima iweke misingi ambayo itawaongoza viongozi
watakaochaguliwa kuacha ubinafsi wa kujali familia zao badala ya maslahi
ya umma.
“Tuwe na Katiba ambayo kiongozi akikabidhiwa madaraka anajua kabisa
kwamba hapa niko kwa ajili ya kuangalia maslahi ya umma, kuna viongozi
badala ya kuhangaika na masuala yanayohusu wananchi wanahangaika na
maslahi binafsi na familia zao,” alisema.
Alisema Katiba iwe na vipengele vya kuhakikisha nchi inakuwa na misingi
ya utawala bora itakayowabana viongozi waroho kutumia madaraka yao
vibaya na kwa maslahi yao.
Alisema hatari anayoiona sasa ni kwa baadhi ya viongozi kuhangaika
kuingiza mambo binafsi yenye maslahi yao ndani ya Katiba badala ya
kuangalia utaifa.
“Tukiacha hali hii iendelee na hawa watu wakachomeka chomeka mambo yao
binafsi mwisho wa siku Katiba hii hii itakuwa chungu kwetu…hata hii
mivutano inayoendelea ya tuwe na marais wangapi kuna watu wanataka
kuingiza maslahi yao hapa,” alisema.
Sitta alisema Katiba mpya lazima ipunguze gharama za uendeshaji na
kuongeza kuwa hata Mawaziri 15 waliopendekezwa kwenye serikali ya
Muungano ni wengi kuliko mahitaji yenyewe.
Alisema mataifa mengi ya Afrika yanatumia fedha nyingi katika uendeshaji
wa serikali wakati wananchi wakiteseka kwenye lindi la umaskini.
“Kama kuna masuala saba tu yanayohusu Muungano, hao mawaziri 15 wote
wanini? Wabunge 150 wote wa kazi gani kama si kufuja uchumi wa nchi,
mimi naona hizi ni mbwembwe ambazo hazina maana sana kwa maendeleo ya
watu,” alisema.
EmoticonEmoticon