Polisi wamsaka Mbowe



Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

Wavamia nyumbani kwake usiku wa manane

JESHI la Polisi nchini linamsaka kwa udi na uvumba Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kwa ajili ya mahojiano. Tayari usiku wa kuamkia jana maofisa wa ngazi za juu wa Jeshi hilo walivamia nyumbani kwake, maeneo ya Mikocheni, Jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kumkamata, lakini walimkosa.
Taarifa ambazo MTANZANIA Jumapili lilizipata tangu juzi kwa makachero wa Jeshi hilo, zilieleza kuwa Polisi walianza kumtafuta Mbowe tangu juzi mchana, lakini bado haikufahamika sababu za kutafutwa kwake.

Taarifa ambazo bado hazijathibitishwa, lakini gazeti hili limezipata kutoka kwa makachero hao, zinaeleza kuwa sababu ya kumsaka Mbowe ni kutaka kumhoji kuhusu tukio la bomu lililotokea Arusha.

Hata hivyo, haikueleweka mara moja kama tukio la sasa la Polisi kuvamia nyumbani kwake linatokana na kauli yake kwamba anao mkanda wa video unaomuonyesha askari wa FFU akirusha bomu.

Taarifa nyingine zilieleza kuwa kitendo cha Mbowe kusakwa na jeshi hilo, kinatokana na mkakati uliotangazwa na Chadema wa kukisuka upya kwa kukipatia mafunzo maalumu kikosi chake cha Red Brigade.

Akithibitisha taarifa za kusakwa kwa mwenyekiti wa chama hicho, Katibu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema Polisi walifika nyumbani kwa Mbowe majira ya saa 6.55 usiku wa juzi kwa ajili ya kuingia kufanya upekuzi wenye nia ya kumkamata.

Dk. Slaa, ambaye alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika viwanja vya Shule ya Msingi Ukombozi, Manzese Jijini Dar es Salaam, alisema operesheni hiyo, iliongozwa na Ofisa Upelelezi Mkoa wa Kinondoni, RCO Ernest Kimola, ambaye alifika nyumbani kwa Mbowe na kulazimisha kuingia ndani ili kufanya ukaguzi wenye nia ya kumkamata.

Slaa alisema, wakati polisi wamevamia nyumbani kwake, Mbowe alikuwa kwenye kazi za chama jimboni kwake Hai, mkoani Kilimanjaro.

“Mbowe ni Mbunge na mfanyabiashara ambaye yupo, anakwenda wapi usiku, wakati wanajua sehemu ya kumpata, nikiwa katibu hakuna ‘summons’ iliyotolewa kuwa anahitajika wala kwenye biashara zake, polisi rudini shule, sheria inasema hakuna ruksa ya kumkamata mtu zaidi ya saa 12 jioni,” alisema Dk. Slaa.

Slaa alihoji uhalali wa jeshi hilo kumtafuta kiongozi huyo mkubwa kama mwizi nyumbani kwake majira ya usiku.

Tukio la polisi kumsaka Mbowe linakuja baada ya wataalamu kutoka nje ambao ni makachero wa upelelezi wa Shirika la Kijasusi la Marekani (FBI) kutua nchini wiki iliyopita, kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo la bomu kwenye viwanja vya Soweto, jijini Arusha.

Katikati ya wiki hii, Mbowe akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio yaliyofikiwa na Kamati Kuu ya chama chake, iliyokutana kwa dharura kwa muda wa siku mbili Julai 6 na 7 mwaka huu, kuwa kutokana na matukio ya kigaidi na mengine ya ukiukwaji wa haki za binadamu aliyodai kuwa yanafanywa na baadhi ya viongozi wa serikali pamoja na wa CCM, sasa umefika wakati wa kuchukua hatua badala ya kuendelea kulia.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kukisuka upya kikosi cha Red Brigade, kwa kukipa mafunzo ambayo ni maalumu kwa ajili ya kujihami.

Mbowe alisema kikosi hicho kitakuwa na shughuli maalumu ya kukabiliana na vitendo vya fujo vinavyofanywa na vijana wa CCM dhidi ya wagombea, wanachama na viongozi wa Chadema.

Hata hivyo wakati taarifa zikidai kuwa Chadema kinajiandaa kuanza kwa makambi hayo wiki ijayo, tayari Jeshi la Polisi lilishaonya kuhusu suala hilo na kuahidi kulifanyia uchunguzi wa kina kwamba haliruhusiwi kisheria.

Gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camilius Wambura, ambaye alishindwa kukiri ama kukataa kwa kudai kuwa uwezo wa kufanya hivyo kwa jeshi hilo upo.

“Achana na hayo mambo … tuongee masuala mengine, waache na propaganda, uwezo wa kufanya hivyo tunao,” alisema kwa kifupi RPC Wambura.
Previous
Next Post »