Msichana wa miaka 19 amechomwa moto hadi kufa na mama yake kupigwa baada ya kuwaomba wazee wa kijiji kuruhusiwa kuolewa na mvulana mmoja kutoka kijijini hapo na ukoo mmoja, polisi wa India wamethibitisha.
Anju Yadav, kutoka kijiji cha Karahkol, wilayani Deoria katika jimbo la Uttar Pradesh, alichomwa moto nyumbani kwake wakati mama yake, Gyanwati Devi, mwenye miaka 48, alipokuwa upande mwingine wa kijiji hicho akiiomba halmashauri ya kijiji kumruhusu Anju aolewe na rafiki yake wa kiume aliyekuwa na mahusiano naye kwa miaka miwili, Ranjit Yadav, mwenye miaka 21.
Lakini halmashauri ya kijiji hicho, sambamba na baba wa mvulana huyo, Jai Hind Yadav, mwenye miaka 52, walitupilia mbali maombi hayo wakisisitiza ilikuwa kinyume cha utamaduni.
Badala yake, baba wa mvulana huyo alikimbilia kwenye nyumba ya familia na kumchoma moto msichana huyo, ilidaiwa.
Jamii ya India inafahamika mno kwa mfumo wake wa ukoo ulioingiliana, ambao unaweza kuzuia watu kutoka jamii tofauti kuoana na katika baadhi ya matukio kuafikiana na jambo kama hilo.
Hatahivyo, inaeleweka kwamba haikubaliki kwa watu kutoka ukoo mmoja na kijiji kuoana. Ndoa ndani ya Gotra (ukoo) mmoja pia hairuhusiwi katika utamaduni wa India, hasa katika mikoa ya kaskazini mwa nchi hiyo ambako makundi ya kiukoo, yanayofahamika kama Khap Panchayats, yanachukulia ndoa kama hizo kuwa kosa la jinai.
Rakesh Kumar, mkuu wa Kituo cha Polisi cha Ikauna, alisema: "Jai Hind pamoja na wanakijiji wengine watatu walikimbilia nyumbani kwa msichana huyo na kumwagia mafuta na kisha kuchoma moto wakati mama yake akiwa kwenye kikao hicho cha halmashauri. Tumewakamata wafuasi wawili wa kundi hilo wakati wengine wawili wakiwa wanaendelea kusakwa."
Anju aliungua asilimia 85 ya mwili wake wote na alifariki dunia akiwa njiani kupelekwa hospitali Alhamisi jioni.
Anju alikuwa peke yake wakati wanaume hao wanne walipovamia nyumbani kwake. Katika kuchanganyikiwa aliruka kutoka kibarazani kwake hadi ghorofa ya pili kujaribu kujiokoa. Alivunjika mikono na miguu yake.
Wanakijiji walimmwagia maji, lakini wakati huo alikuwa tayari amepata majeraha makubwa ya moto.
Mama yake, Gyanwati, alisema wote binti yake na Ranjit walipendana sana na kudhamiria kufunga ndoa.
Gyanwati alikwenda nyumbani kwa Jai Hind Jumatano jioni kujadiliana kuhusu suala la ndoa lakini pale yeye na familia hiyo walipokataa alikwenda katika baraza la kijiji kwa msaada, jambo la kawaida katika India.
Gyanwati alisema: "Nilitaka kumwona binti yangu akiwa mwenye furaha. Walipendana mno; sikuwa na tatizo na ndoa yao. Lakini pale nilipokwenda kwa Jai Hind na maombi hayo alinieleza ni dhambi kuoana ndani ya ukoo mmoja na hatokubaliana na ndoa hiyo."
Polisi wamethibitisha kwamba Jai Hind bado hajapatikana
SOURCE:JAMBO TZ
EmoticonEmoticon