WATOTO ELFU 10 WAPATIWA MATIBABU, PANGANI


Dk. Julius Massaga - Mkurugenzi NIMR
Zaidi ya watoto  elfu kumi walio na umri kati ya miezi 3 hadi miaka 5 wamepatiwa matibabu bure kutoka vijiji 16 vya Wilaya ya Pangani mkoani Tanga.
                                   
Mapema leo mkurugenzi wa Kuratibu na Kukuza Utafiti kutoka NIMR, Dk. Julius Massaga amesema zoezi hilo limefanikiwa kupitia wahudumu wa afya za Msingi na lilikuwa likiwahusu zaidi   watoto waishio katika maeneo ambayo upatikanaji wa huduma za afya ni duni.
 
Kauli hiyo imetolewa wakati wa Mkutano wa 27 wa Taasisi ya Taifa ya utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Tanzania (NIMR) unaofanyika sambamba na na Kongamano la pili la Wanasayansi watafiti barani Afrika, kwa siku nne jijini Arusha Tanzania.
 
Dkt.Massaga amesema watoto hao wamefaidika kwa kupatiwa matibabu bure kupitia mradi unaoendeshwa chini ya NIMR ambao umelenga kupambana na kuepusha vifo vinavyotokana na Malaria ndani ya Wilaya ya Pangani.
 NIMR ilitoa mafunzo na vifaa kwa wahudumu wa Afya 59 lakini kwa uchache wao wameweza kuleta mafanikio kwa mradi huo na jamii kwa ujumla.
 Awamu ya pili ya mradi huo inataraji kuanza mwezi Mei 2013 hadi Mei 2014 na utasaidia pia kutoa elimu dhidi ya Malaria kwa kaya mbalimbali.

Watafiti wanasayansi zaidi ya 300 wa magonjwa ya binadamu na wanyama kutoka Tanzania na nchi mbalimbali duniani wanashiriki kongamano hilo na mada 174 zinawasilishwa na kati ya mada hizo 42 zinajadili umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta za Afya,Mifugo,Wanyapori na Mazingira katika kuthibiti magonjwa ya mlipuko.
Kauli mbiu ya Kongamano hilo la pili barani Afrika la Afya moja ni Mabadiliko ya mandhari ya tafiti za afya barani afrika.
Previous
Next Post »