Muuza dawa za kulevya aliyeishia kukatwa mkono, mguu (2)


Alizamia kwenda katika nchi kadhaa kujihusisha na biashara chafu ya dawa za kulevya.

Katika toleo la jana tuliangalia namna Bembele alivyokuwa na ndoto za kuzamia, kisha akafungwa. Leo tunaendelea; Kwamba licha ya kukamatwa na kuonja chungu ya kuzamia nchi za nje, Mbembele bado alidhamiria kufanikisha lengo lake la kuishi Ulaya kwa kufanya biashara yoyote ile iwe safi au chafu, akiamini hiyo ndio njia ya kumuwezesha kuwa na maisha bora.

“Mwaka 1988 nilikwenda Mombasa Kenya na meli iliyokuwa imebeba mzigo kutoka Tanzania, baada ya kufika huko, viongozi wa ile meli walitushusha na kutuacha pale bila maelezo.”
  Nilikaa pale kwa takriban siku mbili, nilifanikiwa kupata kibarua ndani ya meli ya Kiyogoslavia iliyokuwa inapakia mzigo kuelekea Pakistan,” Mbembele anasema na kuongeza kuwa alipata kibali cha kufanya kazi ndani ya meli hiyo iliyokuwa imeandikwa maandishi makubwa ubavuni ‘Sandra Benz’.
“Baada ya kufanya kazi ya kupakia mizigo mpaka karibu inaisha, nilitafuta sehemu nzuri ya kujificha ili nisionekane na maofisa wa meli hiyo.”

Anasema baada ya kutembea mpaka sehemu ya chini ya meli hiyo, aliona sehemu iliyokuwa na mabomba na mitambo mbalimbali ya meli iliyotota maji machafu yenye mchanganyiko na mafuta ya kupoozea mitambo ya meli.

“Nilipatazama mara kadhaa mahali pale, huku nikijishauri nifanyeje niweze kujificha ili hatimaye nifike Pakistan ambako meli ilkuwa inaenda,” anasema.
             
Alitafuta sehemu ambayo aliweza kukaa juu ya moja ya mabomba hayo bila kulowana wala kuonwa kwa urahisi na walinzi wa meli.
“Kwa kawaida meli ilitakiwa  kuchukua siku saba kufika mjini Karachi Pakistani lakini tulisafiri kwa takriban siku 12”
Akiwa amejificha sehemu ile walikuja watu wengine nao waliokuwa wanataka kuzamia ambao walikuwa ni raia kutoka Kenya, Tanzania na Mauritius hata hivyo hakuwafahamu majina yao.
Wakiwa ndani ya meli wakisafiri kuelekea Pakistan, walikuwa kitu kimoja na wazamiaji wale wengine, waliweza hata kugawana chakula kidogo walichokuwa nacho.
“Kuna siku ilikuwa inapita bila kupata japo mlo mmoja, fikra kubwa ilikuwa ni kwamba tulifika tunakoenda maisha yetu yangekuwa safi”
Akiwa ndani ya meli hiyo hakufanikiwa kuliona jua, alikuwa hatambui ni nyakati gani za siku kwani usiku na mchana vilionekana kuwa sawa kutokana na mahali alipojificha kuwa giza.
“Taa zilizokuwamo ndani ya meli hiyo zilitupa nuru lakini hazikuweza kutusaidia kugundua ni wakati gani wa siku kuwa ni asubuhi, mchana, au usiku” anasimulia.
Kadri siku zilivyokuwa zinaenda, alijifunza kubaini nyakati za siku kwa kuhusianisha matendo ya watu waliokuwa wakifanya kazi ndani ya meli hiyo.
Previous
Next Post »