Mafuriko: Tutaacha lini kumsingizia Mungu


Dar es Salaam. Kila wakati mtu anapopoteza maisha au kupatwa na jambo lolote baya, iwe kwa ugonjwa, ajali ama kuuawa kwa makusudi na watu, kauli ya kuwa kazi ya Mungu haina makosa utaisikia kutoka kwa ndugu na waombolezaji mbalimbali.
Kwa maana hiyo basi, nikisema Watanzania tuna kilema cha kumsingizia Mungu kwa kila jambo linalotupata nitakuwa sijakosea.
Usiku wa kuamkia Disemba 21 mwaka 2011, ilinyesha mvua kubwa jijini Dar es Salaam ambayo ilisababisha mafuriko yaliyopoteza maisha ya zaidi ya watu 40 na wengine zaidi ya 5,000 kukosa makazi.
Wengi walioathiriwa na mafuriko haya ni wakazi wa mabondeni hususani eneo la Jangwani, mto Msimbazi na Kigogo.
Ikiwa ni miaka miwili, miezi mitatu na siku tatu tangu kutokea kwa mafuriko hayo Dar es Salaam, juzi ilikumbwa tena na mafuriko mengine yaliyotokana na mvua zilizonyesha katika maeneo mbalimbali ya Jiji.
Wakati wa mvua za mwaka 2011 Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), walitabiri kutokea kwa mvua hizo na kuwataka watu wa mabondeni wachukue hatua ikiwa ni pamoja na kuhama.
Viongozi mbalimbali wa mkoa pia waliwataka watu wanaoishi kwenye maeneo hatari kuhama, lakini kwao maelezo yote yalikuwa ni kama kelele za chura ambazo Waswahili wanasema hazimnyimi usingizi mwenye nyumba.
Madhara hayo yametokea siku moja baada ya dunia kuadhimisha siku ya hali ya hewa (23 Machi), iliyokuwa na kauli mbiu ya “Ufuatiliaji wa hali ya hewa ili kulinda maisha na mali”
Vivyo hivyo mvua za juzi zimetokea wakati ambapo TMA walishatabiri kuwapo kwa mvua kubwa.
Utamaduni wetu ni kukaa kimya bila kusikiliza ni nini utabiri wa hali ya hewa unasema, baada ya ndugu zetu kupoteza maisha kutokana na mafuriko tunabaki kusema kazi ya Mungu haina makosa, siyo kweli tunamsingizia Mungu.
Siku chache baada ya mafuriko ya mwaka 2011, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, iliazimia kubomoa nyumba zote zilizojengwa mabondeni, katika kipindi cha mwezi mmoja, ukiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Kikwete.
Siku tatu kabla ya kauli hiyo ya Halmashauri, Rais Jakaya Kikwete, alitembelea Shule ya Msingi Mchikichini kwa lengo la kuwapa pole watu walioathiriwa na mafuriko hayo na kuwataka wanaoishi mabondeni kuhama mara moja, ili kuepuka kupoteza maisha na mali zao.

 


 
Previous
Next Post »