TATIZO la upungufu wa chakula limeyakumba maeneo mengi nchini na sasa kuna baadhi ya maeneo wananchi wameanza kula mizizi.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi unaonyesha kuwa baadhi ya maeneo yaliyoathirika kwa njaa kuwa ni pamoja na Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha, Handeni na Kilindi mkoani Tanga, Nkasi mkoani Rukwa na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Shinyanga.
Wilayani Ngorongoro hali ni mbaya zaidi katika Tarafa ya Ngorongoro, ambako idadi kubwa ya watu wa eneo hilo, wanaishi kwa kula matunda na mchicha wa porini.
Tarafa hiyo iliyopo ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, ina wakazi wanaofikia 70,000, ambao ni wafugaji wa jamii ya Kimasai waliohamishiwa kwenye eneo hilo kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wakati ilipoanzishwa.
Eneo hilo lenye njaa ni moja ya maeneo maarufu duniani yaliyotangazwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuwa ni eneo la urithi wa dunia.
Kwa sasa eneo hilo, linaingiza kiasi cha Sh52 bilioni kwa mwaka, ikiwa ni mapato yanayotokana na watalii wanaoingia kwenye hifadhi.
Kinachowavutia watalii kutembelea eneo hilo, pamoja na vivutio vingine vya utalii ni kuangalia maisha ya watu wa jamii ya Kimasai wanavyoishi pamoja na wanyamapori kwenye kasoko (shimo la volcano).
Hali ya njaa kwa sasa
Pamoja na kuwa eneo hilo linakabiliwa na njaa, kumekuwapo na mvutano baina ya baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Arusha, Wilaya ya Ngorongoro pamoja na Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) juu ya ukweli kuwapo kwa njaa.
Kila upande umekuwa na tamko lake kuhusiana na tatizo la njaa Ngorongoro.
Wakati Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo akisema eneo hilo, linakabiliwa na upungufu wa chakula, Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, Saning’o Ole Telele pamoja na NGO’s wanasema eneo hilo lina njaa kali.
Hata hivyo, Mwananchi hivi karibuni ilitembelea vijiji vya Kata za Nainokanoka, Enduleni, Alailelai na Kata ya Ngorongoro na kushuhudia watu wengi katika wilaya hiyo wakikabiliwa na njaa.
Kijana mlinzi wa miaka 18 analea familia ya watu 16.
Moja ya familia, ambayo inakabiliwa na njaa katika eneo hilo ni ya kijana Menguru Parisani (18), yenye watu 16, wengi wakiwa wanawake na watoto.
Hata hivyo, Perisani mwenyewe amelazimika kwenda jijini Mwanza kufanya kazi ya ulinzi, ili apate fedha za kulisha familia.
Baada ya kufika nyumbani kwa Perisani, mwandishi wa habari hizi alikutana na wanawake wawili, waliokuwa wakijiandaa kwenda kusaga wastani wa kilo tano za mahindi.Nahoro Ngidadya ni mama wa watoto wanne katika familia hiyo, aliyejitambulisha kuwa ni mjane, ambaye mumewe alifariki katika ajali ya gari, hivi karibuni akiwa anafanya kazi ya kibarua.
Anaeleza kuwa mwanamume huyo, alipofariki alimwacha na ng’ombe mmoja ambaye ndiye wamekuwa wakimtegemea kwa kupata maziwa wanayokunywa.
Huku akionekana kukata tamaa, anasimulia kuwa maisha yake ya kila siku na watoto wake yamekuwa magumu.
“Watoto wangu Nasabuko, Chinene bado ni wanafunzi, Oturohu na Laitelei hawajaanza masomo wakiamka asubuhi nimekuwa nikiwapa chai ya maziwa isiyo na kitafunwa, wanakwenda shule na wakirudi mchana nawakorogea uji, wanaokunywa pamoja na kuwachemshia mchicha pori au mnafu,” anasimulia mama huyo.
Huku akionyesha mboga hizo, zinazopatikana katika mapori ndani ya tarafa hiyo, Ndidadya anasema kuwa kwa zaidi ya wiki mbili sasa, amekuwa akiwapa watoto uji na mboga hizo.
“Kuna wakati watoto hawa hukosa nguvu na hupata kizunguzungu, lakini sina cha kuwapa zaidi ya uji, kwani siwezi kutumia unga kidogo nilionao kuwasongea ugali,” anasema Ndidadya.
Mwandishi alishuhudia watoto wa familia hiyo wakirejea kutoka shuleni mchana wakiwa wamechoka, huku wazazi wao wakisubiri kusaga mahindi kabla ya kurejea na kuwakorogea uji.
Naye Noondomono Parsani anayetoka katika familia hiyo, akiwa na watoto watatu, awali anakataa kuzungumza akieleza haelewi lugha ya Kiswahili lakini anajitokeza mkalimani na kutuwezesha kuwasiliana.
Parsani anaeleza kuwa maisha yao ni duni na kila siku hawajui kesho yao itakuwaje na kwamba licha ya kupewa mahindi ya msaada, debe moja limeshindwa kusaidia familia yao.
“Sasa wanakupa debe moja kwa miezi miwili, utakulaje? Ni bora tu kupika uji kwani ugali unatumia unga mwingi,”anasema Parsani
Anasema kuwa ingawa kwa sasa kuna mahindi yanayouzwa Sh9,000 kwa debe, lakini familia yao haina uwezo wa kununua, kwa kukosa fedha, wala ng’ombe wa kukamua ili wauze.
“Hata kama tungekuwa na ng’ombe wa kutosha kukamua maziwa, sasa huku utamuuzia nani maziwa. Kikubwa, huku tupate chakula tu, kwani kilimo kimezuiwa,” anasema Parsani.
Kutokana na hali ya familia hiyo, mwandishi alilazimika kuisaidia familia hiyo kwa kuipa fedha kidogo ili wanunue mahindi na baadaye kwenda katika familia nyingine.
Lita moja ya maziwa yaokoa maisha ya wajukuu.
Katika familia nyingine eneo la Nainokanoka, mwandishi alikutana na Naromay Lembirika aliye na umri unaofikia miaka 65, akiwa amekaa barabarani na kidumu kidogo cha lita moja ya maziwa.
Baada ya kumuuliza alisema kuwa anauza maziwa hayo, Sh500 kwa lita moja, lakini amekaa njiani hapo kwa zaidi ya saa tatu, bila kupata mteja.
“Nipo hapa nakaa tu, nasubiri mtu wa kununua maziwa, nikipata fedha hii naenda kununua mahindi, nisage nipeleke nyumbani,” anasema Lembirika.
Anasema nyumbani ana wajukuu saba, alioachiwa na watoto wake, ambao wameenda mjini kutafuta kazi za ulinzi.
“Nikipata fedha na mahindi kopo moja, basi nasaga unga huwapikia watoto uji wanaokunywa mchana,” anasema Lembirika.
Anasema wajukuu zake sasa wameanza kuzoea maisha hayo ya dhiki, kwani siku nyingine anakosa mteja wa maziwa na kurudi nyumbani na maziwa, ambayo huchemsha na kuyaongezea mchicha pori kisha kuwapa watoto ili wanywe.
Kwa hali ya bibi huyu siwezi kuondoka hivi hivi, nalazimika pia kumpa fedha kidogo walau akanunue mahindi anapokea na kuniombea dua japo kwa lugha ya Kimasai.
Next
« Prev Post
« Prev Post
Previous
Next Post »
Next Post »
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
EmoticonEmoticon