Mbaroni akidaiwa kumkata ulimi ‘wifi’

MWALIMU wa Shule ya Msingi Mfaranyaki iliyopo Manispaa ya Songea, Theresia Fuli anashikiliwa na polisi kwa kosa la kumjeruhi kwa kumng’ata ulimi hadi kukatika wifi yake kwa wivu wa mapenzi.
Akizungumza kwa tabu  kwenye hospitali ya mkoa alikolazwa wodi daraja la kwanza kwa ajili ya matibabu, majeruhi huyo Oliga Msigale mkazi wa Msamala amesema, bado ana maumivu makali ya ulimi ingawa amepatiwa matibabu.
Amesema siku ya tukio alishangaa kuona anavamiwa na wifi yake ambaye ni mtalaka wa kaka yake, ambapo alimtupia mtoto mkubwa wa kaka yake maharage ya moto kisha kumvamia yeye, huku akimtuhumu kuwa ndiye binti ambaye amechukua nafasi yake bila kujua kuwa yeye ni ndugu wa mume na alipoanguka chini alikabwa koo na alipotoa ulimi nje mwanamke huyo bila huruma alimngata ulimi na kutoa kipande cha ulimi kisha akatoroka eneo hilo.
Amesema mara baada ya tukio hilo, alisikia maumivu makali na alikimbizwa hospitalini ambapo walipitia polisi kutoa taarifa na mtuhumiwa alikamatwa, lakini baadaye alipata dhamana baada ya kudanganya kuwa anaumwa hivyo kulazwa Peramiho.
Baadhi ya mashuhuda akiwamo jirani wa binti huyo, ameeleza kuwa siku ya tukio walishangaa kuona mwanamke huyo akiwa amefura kwa hasira.
Kutokana na kuwa alikuwa ameachana na mumewe kipindi kirefu,
alipopata taarifa kuna binti anaishi kwa mumewe moja kwa moja alidhani ni mke mwenzie hivyo alimvamia na kumuuma ulimi kisha akakimbia.
“Huyu mwanamke aliyefanya unyama huu alikuwa mke wa ndoa wa kaka yake, lakini aliamua kumpa talaka kaka wa huyo binti ili awe huru, kutokana na kutowajua ndugu wengi wa upande wa mumewe aliposikia kuna binti anaishi na mumewe alichukia na kuja kunishambulia bila kujua huyo yupo pale kwa ndugu yake kwa ajili ya kulea watoto na si vinginevyo,”alisema.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, George Chiposi amekiri kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema tukio hilo liliripotiwa polisi na Ayub Joseph( 18) mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Msamala.



 

Previous
Next Post »