JK awatosa CC wawania urais 2015


MWENYEKITI wa CCM, Rais Jakaya Kikwete

MWENYEKITI wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ameamua kuwatosa vinara wanaotajwa kutaka kuwania urais kupitia chama hicho kutoingia kwenye Kamati Kuu (CC).
Dalili za kuwatosa vinara wanaotajwa kuwania urais 2015, ni kutokana na hatua yake ya juzi kuamua kutowapendekeza kuwa miongoni mwa majina ambayo yangepigiwa kura ili kuweza kuingia katika CC.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa ndani na nje ya CCM wanaona hatua ya Kikwete kutopendekeza majina ya wanasiasa vigogo wanaotaka urais 2015 kupitia chama hicho katika orodha ya watu 42 ili kuwania nafasi 14 za CC kama mkakati maalumu wa kuwaweka kando.

Hata hivyo, mkakati huu wa Kikwete ulikuwa hatua muhimu kwake kama kiongozi wa chama baada ya kukwama kuzuia makundi kung’ara katika chaguzi zilizopita ambapo wafuasi wa Edward Lowassa waliibuka kidedea kuanzia katika NEC, mikoani na Jumuiya za chama hicho.
Ndiyo maana baada ya kumalizika Uchaguzi wa wajumbe wa NEC, Kikwete alisita kuunda CC kwa maelezo kwamba waliochaguliwa walikuwa wageni na alikuwa hawafamu vizuri. Hatua hii ya Kikwete ilitafsiriwa kama mkakati wa kuzima nguvu ya mojawapo ya kambi.
Hata hivyo, kuna mtazamo tofauti kwamba hatua ya Kikwete kutopendekeza majina makubwa na yenye nguvu ndani ya CCM kuwania ujumbe wa Kamati Kuu inaweza ikawa ni njia ya kuwafanya wajumbe wa CC kuwa na kazi moja tu ambayo ni kuchuja majina ya wagombea badala ya wao pia kuwa washiriki.


Kutoswa kwa vigogo
Katika hali iliyozua gumzo, majina ya wanasiasa vigogo Edward Lowassa, Benard Membe na Samuel Sitta ha yakuwamo katika orodha ya Rais Kikwete aliyowasilisha mbele ya NEC ili kupata wajumbe wa CC, ambacho ni chombo muhimu cha uamuzi ndani ya chama hicho.

Lowassa, Membe na Sitta ndiyo wanaelezewa kuwa na makundi makubwa yana yowaunga mkono kiasi cha kutishia uhai wa chama hicho katika chaguzi zijazo.
Makundi ya watu hao yamekuwa hasimu kiasi cha wakati fulani, Kikwete kulazimika kuunda kamati ya watu watatu chini ya Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Makamu Mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Pius Msekwa na Abdulrahman Kinana, ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho kwa sasa ili kusuluhisha mgogoro huo.

Hata hivyo, kansa ya mgogoro imeendelea na kujipambanua waziwazi na hasa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa chama hicho mwaka jana wakati makundi hayo yalipopambana kujaza wafuasi wao kwenye NEC kwa lengo la kujipanga kwa ajili ya uchagzui wa 2015.

Wafuatiliaji wa siasa za CCM wanaamini kukosekana kwa Lowassa, Membe na Sitta bila shaka ni pigo kwa mbio za wanasiasa hao kutaka kuingia Ikulu mwaka 2015.
Kwani kama watapenya kwenye kinyang’anyiro cha kuwania urais kupitia CCM mwaka 2015 watakuwa wamefuata nyayo za Benjamin Mkapa ambaye aliteuliwa kugombea urais akiwa si mjumbe wa CC


Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na Kikwete walikuwa wajumbe wa CC kabla ya uteuzi wao kugombea urais.

Maoni ya watu mbalimbali
Baada ya CCM kuhitimisha safu yake ya uongozi kwa Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC) kuchagua wajumbe CC huku kikiwatosa wanaotajwa kutaka kuwania urais 2015, baadhi ya wasomi wamesema kitendo hicho kinaonyesha kuwa chama hicho tawala kimedhamiria kujiimarisha.

Wakitoa maoni kwa nyakati tofauti wasomi hao walisema hali ingekuwa mbaya ndani ya chama hicho kama baadhi ya watu hao wangechaguliwa kuwa wajumbe wa CC.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Profesa Gaudence Mpangala alisema kutopendekezwa kwa Lowassa, Membe na Sitta kulitarajiwa kwa kuwa viongozi wengi wa chama hicho walikuwa hawapendi jinsi baadhi ya wanachama wa CCM wanavyoonyesha wazi dhamira yao ya kuutaka urais.
 
Previous
Next Post »