Hofu ya ghasia katika uchaguzi wa Kenya

Shirika la kutetea haki za binadamu la, Human Rights Watch limeonya kuwa uchaguzi mkuu wa mwezi ujao, nchini Kenya huenda tena ukakumbwa na ghasia.

Kwa mujibu wa shirika hilo, maafisa wa serikali wamekosa kuchukulia kwa uzito sababu zilizosababisha ghasia za mwaka 2007, na kuweza kuzishughulikia. Maelfu ya watu waliuawa kwenye ghasia hizo.

Shirika hilo linasema kuwa serikali ya Kenya bado haijafanya mageuzi muhimu, na imekosa kushughulikia vyanzo vya ghasia nchini humo.

Limeelezea mfano wa ghasia za kikabila ambazo zimekuwa zikiendelea kama zile zilizoshuhudiwa Tana River, ukosefu wa mageuzi katika idara ya polisi, pamoja na kukosa kushughulikia maswala ya ardhi ambayo yamekuwa sababu kuu ya mizozo katika nchi hiyo.

Pia serikali imekosa kuwachukulia hatua washukiwa wa ubakaji, mauaji na ghasia nchini humo.

Shirika hilo linadai kuwa jamii fulani tayari zimeanza kujihami kwa hofu ya mashambulizi kabla ya uchaguzi mkuu likisema kuwa madai haya yanaweza kuthibitshwa kwa sababu ya taarifa zilizokusanywa na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali.

Kwenye ripoti ya shirika hilo, katika baadhi ya sehemu za nchi kuna hali ya wasiwasi na hofu ya ghasia.

Ghasia zilizotokea wakati wa uchaguzi wa 2007 na 2008 zilitikisa sifa ya Kenya iliyokuwa inatazamiwa kama nchi thabiti na mfano mzuri kwa Afrika Mashariki, wakati kilichoanza kama vurugu la kisiasa kugeuka na kuwa ghasia za kikabila zilizosababisha vifo vya watu 1,200 na kuwaacha wengine 600,000 bila makao.

Wasiwasi hasa umeongezeka kwa sababu ya kesi za washukiwa wa ghasia za baada ya uchaguzi huo zinazotarajiwa kuanza kusikilizwa katika mahakama ya Hague.
Previous
Next Post »