Waziri Mkuu Mizengo Pinda akitaka maelezo zaidi kuhusu aina ya mbegu ya mahindi iliyotumika kutoka kwa Bi. Grace Hokororo ambaye ni Bibishamba wa kata ya Itenka wakati alipokuwa akikagua shamba darasa analolisimamia kwenye kijiji cha Itenka wilayani Mlele, Katavi, jana jioni (Januari 6, 2013). Alifurahia kazi yake na kuahidi kumpatia pikipiki imsaidie kutembelea vijijiji vingine vinne anavyovisimamia. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Bibishamba wa kata ya Itenka, Bi. Grace Hokororo akipokea zawadi ya sh. 305,000/- kutoka kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambazo zilichangwa papo hapo na watu alioandamana nao ili kumpongeza kwa kazi nzuri aliyoifanya kwenye shamba darasa. Wa pili kulia ni Bw. Joseph Laurent anayesimamiwa na bibishamba huyo ambaye shamba lake lilikaguliwa na Waziri Mkuu katika kijiji cha Itenka jana jioni (Januari 6, 2013) wilayani Mlele, Katavi. Pia aliahidiwa kupatiwa pikipiki ili imsaidie kutembelea vijijiji vingine vinne anavyovisimamia. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*Amsifu kumkuta akiwa amevaa unifomu, asifia shamba darasa analolisimamia
*Achangiwa sh. 505,000/ za papo hapo
*Wanakijiji walitaka kumtosa wakidai hawamjui
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amekunwa na utendaji kazi wa Bibi Shamba wa kata ya Itenka, Bi Grace Hokororo na kuamua kumpa zawadi ya pikipiki ili imsaidie kuzungukia vijiji anavyovihudumia.
Waziri Mkuu alitoa ahadi hiyo jana jioni (Jumapili, Januari 6, 2013) mara baada ya kukagua shamba la mfano katika kijiji cha Itenka B, kata ya Itenka, wilayani Mlele, mkoani Katavi. Kabla ya hapo, Waziri Mkuu alihutubia mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya shule ya msingi ya Itenka B.
Kabla ya kuamua kukagua shamba darasa la mkulima anayesimamiwa na Bibi shamba huyo, Bw. Joseph Laurent, wakiwa kwenye mkutano wa hadhara, wakazi wa kata hiyo walitaka kumtosa bibi shamba huyo kwa kudai kwamba hawamjui na hawajawahi kuona shamba darasa lolote.
Sekeseke lilianza wakati Waziri Mkuu alipokuwa akisisitiza matumizi ya kilimo cha sesa na kuhoji kama wakazi hao wanaye bwanashamba, ndipo walipojibu hawana. Bi. Hokororo alipojitokeza wakadai hawamjui, alipoulizwa na Waziri Mkuu kama ana ushahidi wowote, Bi. Hokororo akataja vijiji anavyovisimamia ambavyo ni Itenka “A”, Itenka “B”, Diripu, Tumaini na Tukoma.
Bi. Hokororo (26) ambaye amefanya kazi kwenye kata hiyo kwa mwaka mmoja na hana usafiri, aliokolewa na wakulima wachache ambao walijitokeza na kukiri kuwa wamefundishwa kilimo bora kwenye mashamba yao na kusimamiwa na bibi shamba huyo.
Ndipo Waziri Mkuu alipomchagua Bw. Laurent na kumuuliza shamba lake liko wapi. “Liko hapa hapa kijijini, amenisadia na sasa hivi ninavuna magunia 30 kwa ekari moja” alijibu Bw. Laurent mwenye ekari tatu na kumfanya Waziri Mkuu aamue kwenda kulikagua.
Akiwa shambani hapo, alishangaa kukuta mahindi yamepandwa kwa mistari, yamepaliliwa vizuri na yamewekewa mbolea naye bila kuamini alichokiona, huko huko shambani, akaahidi kumpatia pikipiki ili imsaidie katika kazi zake.
“Kwanza huyu ni bibi shamba wa kwanza kumkuta akiwa na unifomu… shamba zuri, limepandwa kisasa kabisa, mahindi yamepaliliwa na tena yana mbolea. Ni mazuri kabisa! Nitampatia pikipiki mara moja,” alisema Waziri Mkuu ambaye alikuwa anamalizia ziara yake ya jimbo kwenye kata mbili kati ya 14 zilizobakia wakati wa ziara yake Desemba, mwaka jana.
Kabla ya kutoka katika shamba hilo, mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda alikusanya michango ya papo hapo ikiwa ni zawadi kwa bibi shamba huyo na kufanikiwa kukusanya sh. 305,000/- zikiwa ni fedha taslimu ambazo alimkabidhi hapo hapo shambani. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, Bw. Estomih Chang’a aliahidi kumpatia sh. 200,000/- kabla ya mwisho wa wiki hii.
EmoticonEmoticon