Wanajeshi wa Mali wawabana waasi


wanajeshi wa Mali
Majeshi ya Mali, yameutwaa mji muhimu wa Douentza, ulio katikati ya nchi hiyo, kutoka kwa wapiganaji wa Kiislam.

Hii ni mara ya kwanza kwa jeshi hilo kudai kuurejesha mji uliokuwa umekaliwa na wapiganaji wa Kiislam kaskazini mwa nchi.

Habari zimesema, jeshi la Mali pia limeanzisha operesheni ya kijeshi kuurejesha mji wa Konna.

Jumanne, wiki hii, mwenyekiti wa Muungano wa Afrika, Thomas Boni Yayi, amesema NATO itatakiwa kutuma majeshi yake nchini Mali kupambana na wapiganaji wa Kiislam.

Amesema mgogoro wa Mali, ni mgogoro wa dunia ambao NATO inatakiwa kuingilia kati kama ilivyofanya nchini Afghanistan kukabiliana na vikundi vya Taleban na al-Qaeda.

Mwanajeshi wa Mali akiwasaka wapiganaji wa waasi

Amesema, vikosi vya Nato vitatakiwa kushirikiana na majeshi ya Muungano wa Afrika yaliyoko nchini Mali.

Baadhi ya viongozi wa Ulaya wameelezea wasiwasi kwamba wapiganaji wa kiislam kutoka maeneo mengine duniani, wanaweza kutumia eneo kubwa la Mali, linalodhibitiwa na wapiganaji wa Kiislam, ambalo sawa na ukubwa wa Ufaransa, kufanya mashambulio dhidi ya nchi za Ulaya.

Mwezi uliopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, liliidhinisha mipango ya kupeleka askari 3,000 kutoka nchi za Afrika Magharibi, kupigana dhidi ya wapiganaji wa Kiislma nchini Mali.

Lakini maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesema hawakutarajia upelekaji wa askari hadi mwezi Septemba 2013.

Mapigano makali


Wapiganaji wa waasi wa Mali

Habari kutoka jeshi la Mali zimeiambia BBC, kwamba mji wa Douentza, ulio umbali wa kilomita 800 Kaskazini Mashariki mwa mji mkuu Bamako, yameutwaa kutoka wapiganaji wa Mujao-Movement for Unity and Jihad in West Africa, kufuatia mapigano makali.

Kikundi cha Mujao, hakijazungumzia lolote madai ya jeshi la Mali.

Mujao wamekuwa wakiudhibiti mji wa Douentza tangu Septemba 2012.

Taarifa zinasema jeshi pia limeanzisha operesheni ya kijeshi kuwaondoa wapiganaji wa Kiislam kutoka mji wa Konna, ambao uko pembezoni mwa eneo linalodhibitiwa na serikali na mji mkuu wa jimbo wa Mopti.
Previous
Next Post »